***********************************
SHIRIKA la kimataifa la Uhifadhi (WWF),limetoa elimu na vifaa katika vijiji vitano vilivyoathirika na tembo waharibifu wa mazao Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,ili kuwadhibiti wanyama hao.
Mhifadhi kutoka WWF Deogratias Kilasara amevitaja vijiji vilivyonufaika na mradi huo kuwa ni Misiaji, Mpanju, Malumba,Mbati na Machemba ambapo amesisitiza WWF imedhamiria kuhakikisha tembo waharibifu wanadhibitiwa bila madhara.
‘’Wilaya ya Tunduru imekuwa na matukio mengi ya tembo waharibifu wanaovamia maeneo ya mashamba na makazi ya binadamu,WWF inashirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa haya matukio yanapungua kwa kutoa elimu na vifaa vya kukabiliana na tembo’’,alisisitiza.
Amesema katika msimu uliopita WWF ilitoa elimu ya matumizi ya pilipili na uzio wa kitambaa kwa kutumia mafuta machafu na kutoa matokeo mazuri ambapo amekitaja kijiji cha Misiaji kuwa cha mfano wa kuweka uzio kuzui tembo katika mashamba.
Hata hivyo amesema WWF imetoa mabomu 400 ya kufukuza tembo waharibifu wilayani Tunduru kwa ajili ya matumizi msimu ujao wa kilimo.
Wakizungumza namna walivyonufaika na elimu ya kukabiliana na tembo waharibifu wa mazao katika msimu uliopita,wananchi wa kijiji cha Misiaji Tunduru wamelishukuru Shirika la WWF kwa elimu hiyo ambayo imewawezesha kuvuna mazao yao bila kuathiriwa na tembo.
Said Amigo Mkazi wa Misiaji Tunduru amesema baada ya kupata elimu,aliweka uzio wa pilipili kwenye shamba lake la mahindi na viazi ambapo amefanikiwa kuvuna mahindi gunia 36 na viazi anaendelea kula hadi sasa na kwamba tembo wanafika lakini hawaingii kwenye mashamba yake.
Rashid Kassim Mkazi wa Misiaji na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chingoli Tunduru amesema katika msimu uliopita walifanikiwa kufunga uzio wa pilipili kwenye mashamba ya vijiji vya Misiaji na Malumba kupitia ufadhili wa WWF na kwamba tembo walipofika kwenye mashamba yenye uzio hakuna shamba lililoshambuliwa.
Amesema wakulima kutoka vijiji hivyo wameamini na kuridhika kuwa pilipili na mafuta machafu ni kiboko ya tembo waharibifu wa mazao kwa sababu mazao yao yamesalimika.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Agustino Maneno amewapongeza WWF kwa mafunzo ya kukabiliana na tembo waharibifu ambayo yamewawezesha wananchi kuvuna mazao yao katika msimu uliopita.
“Nawapongeza sana kwa msaada wa mafunzo na mabomu 400 ya kufukuza tembo waharibifu,hata hivyo kwa ukubwa wa wilaya na changamoto iliyopo kwa mwaka walau tunahitaji mabomu 200 kukabiliana na tembo waharibifu’’,alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini Mheshimiwa Daim Idd Mpakate amewashukuru WWF kwa kutoa elimu na vifaa vya kukabiliana na tembo waharibifu ambapo amesema idadi ya tembo watapungua na kwenda kwenye maeneo yao ya asili .
Mbunge wa Tunduru Kaskazini Mheshimiwa Hassan Myao ametoa rai kwa WWF kushirikiana na TAWA TANAPA,TFS na wadau wengine wa mazingira kutafuta njia nyingine mbadala za kukabilina na tembo waharibifu.