Afisa Uendeshaji wa Kampuni ya Serengeti Bytes,Michael Mallya, akizungumza na vyombo vya habari wakati wa uzinduzi wa Tuzo za Tanzania Digital Awards msimu wa mwaka 2021
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti Bytes,Kennedy Mmari akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi wa Tuzo za Tanzania Digital Awards kwa mwaka 2021.
***
Alhamisi, Oktoba 7, 2021 : Msimu wa Tuzo za Digitali (Tanzania Digital Awards) mwaka 2021 umezinduliwa rasmi Alhamisi tarehe 7 Oktoba, 2021 jijini Dar es Salaam. Tuzo za Tanzania Digital Awards zinakusudia kukuza uwajibikaji, ubunifu, na uvumbuzi katika uwanda wa digitali Tanzania.
Msimu wa kwanza wa Tuzo za Digitali 2020 ulipokelewa vizuri na wadau na umma. Mwaka 2020, Tanzania Digital Awards ilipata mapendekezo ya wanaowania tuzo zaidi ya 50,000 huku jumla ya kura zilizopigwa zikiwa ni 150,000 na kupata jumla ya washindi 50. Katika msimu wa kwanza, TDA ilifikia takribani watu 36,000,000 kupitia mitandao na vyombo vya habari ndani na nje ya Tanzania.
Taasisi za umma, makampuni, mashirika yasiyo ya kiserikali, na watu binafsi walipendekezwa na kupigiwa kura katika vipengele 10.
Vipengele vikuu vilivyowaniwa mwaka jana ni pamoja na Serikali Mtandaoni, Diplomasia Mtandaoni, Masoko Mtandao, Burudani Mtandaoni, Vyombo vya Habari Mtandaoni, Uvumbuzi wa Kidijitali, Mawasiliano ya Kidijitali, Uchechemuzi Mtandaoni, Tuzo ya Heshima na Tuzo ya Ujumla ya Chaguo la Watu.
Kufuatia maoni ya wadau mbalimbali, mwaka huu Tanzania Digital Awards imepanua wigo kwa kuongeza idadi ya vipengele vikuu kuwa 12 na vipengele vidogo 52.
Vipengele vikuu vya mwaka 2021 ni pamoja na kipengele cha Uvumbuzi wa Kidijitali, Huduma za Benki Kidigitali, Sekta ya Mawasiliano ya Simu Kidigitali, Mawasiliano Kidigitali, Burudani Kidigitali, Masoko na Biashara Kidigitali, Vyombo vya Habari Kidigitali, Serikali Kidigitali, Uchechemuzi Kidigitali, Diplomasia Kidigitali, Tuzo ya Chaguo la Watu na Tuzo ya Heshima,
Uzinduzi wa msimu wa mwaka 2021 umeenda sambamba na uzinduzi wa mchakato wa mapendekezo ya watakaowania tuzo uliopangwa kuanza Oktoba 7 hadi Novemba 1, 2021.
Mchakato wa kupendekeza wawania tuzo katika kila kipengele utafanywa kupitia fomu maalumu ya mapendezo itakayopatikana kupitia tovuti ya Tanzania Digital Awards.
Mtu yeyote anaweza kupendekeza watakaowania tuzo katika kipengele chochote anachokipenda. Mbali na kupendekezwa, mtu anayefanya vizuri katika matumizi ya technolojia za kidigitali nchini Tanzania anaweza kujipendekeza mwenyewe katika vipengele anavyoona vinafaa.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi jijini Dar es Salaam, Michael Mallya, Afisa wa Uendeshaji wa kampuni ya Serengeti Bytes ambao ni waandaaji wa tuzo hizo alisema wanatarajia msimu wa kusisimua na wenye ushindani zaidi.
“Baada ya kupokelewa kwa mafanikio makubwa mwaka jana, mwaka huu tunatarajia msimu wa kusisimua na wenye ushindani zaidi kwa sababu Watanzania wengi na wadau mbalimbali wametambua thamani ambayo tuzo hizi inaongeza katika mapinduzi ya kidigitali nchini Tanzania. Tunatarajia kupokea idadi kubwa zaidi ya mapendekezo na vilevile wakati wa upigaji kura, tuna hakika kwamba watu watapiga kura kwa shauku ya kuona wanamapinduzi ya kidigitali wakiibuka kidedea,” alisema Bw. Mallya.
Akifafanua mpango wa tuzo za Tanzania Digital Awards 2021, Mallya alieleza kuwa baada ya mchakato wa mapendekezo kufungwa mnamo Novemba 1, jopo la wataalamu ambao wanahusika na tathmini ya jumla ya tuzo watachuja na kupitisha majina ya wawania tuzo katika kila kipengele.
Baada ya kukamilisha mchakato wa kuchagua majina ya watakaowania tuzo, majina hayo yatawekwa kwenye tovuti tayaru kwa ajili ya wananchi kuanza zoezi la upigaji kura ambalo limepagwa kuwanza Novemba 4 hadi 25. Baada ya kumalizika kwa mchakato wa kupiga kura, jopo la wataalamu litaidhinisha washindi tayari kwa ajili ya kukabidiwa tuzo katika hafla iliyopangwa kufanyika Disemba 10, 2021.
“Mwaka jana mambo hayakuenda kama tulivyopanga kwa sababu ya mtikisiko uliosababishwa na mlipuko wa janga la korona lakini mwaka huu tunatarajia kuwaleta pamoja wadau muhimu na washindi wa tuzo kwa lengo la kusherehekea matokeo chanya katika mapinduzi ya kidigitali nchini Tanzania. Tutaendelea kutoa taarifa kwa umma juu ya michakato na matayarisho yote hadi washindi watakapotangazwa, ”alisema Michael.
Kauli mbiu ya msimu wa Tanzania Digital Awards 2021 ni ‘Digitali Kwa Maendeleo’ (Digital For Development) – kauli mbiu hii inalenga kuhimiza ubunifu, uvumbuzi, na uwajibikaji kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Wananchi wote na wadau wanahimizwa kutembelea tovuti www.digitalawards.co.tz kwa taarifa zaidi juu ya vipengele, namna ya kupendekeza, namna ya kupiga kura, na namna ya kudhamini tuzo hizi. Kwa ambaye anahitaji ufafanuzi zaidi anaweza kuwasiliana na waandaaji kupitia barua pepe; [email protected] au kupitia simu; +255 737 957 082.
Tuzo za Tanzania Digital Awards zilizundiliwa rasmi Januari 16, 2020 kwa lengo la kuwatambua watu, taasisi na kampuni zinazotumia teknolojia za kiditali kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Tanzania Digital Awards zinalenga kuchagiza Uwajibikaji, Ubunifu na Uvumbuzi kwenye majukwaa ya Dijitali.
Tuzo hizi huandaliwa na Serengeti Bytes kampuni ya teknolojia, huduma za mawasiliano ya kimkakati, mahusiano na umma na masoko.