SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan, imetenga zaidi ya sh. Trilioni 2.3 za kuwasaidia Watanzania wenye sifa kuondokana na umasikini,haitawaacha nyuma huku ikiiagiza Bodi ya Mikopo kuwapa kipaumbele watoto wa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia TASAF.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa alipowatembelea wanufaika wa mpango huo unaotekelezwa na TASAF, katika Kijiji cha Nyang’homango wilayani Misungwi, Mwanza.
Alisema serikali itaziwashika mikono familia na wananchi wanaokabiliwa na umasikini wa kipato kwa kuwapa ruzuku ya fedha ili kuwawezesha kumudu milo mitatu kwa siku na kuboresha maisha yao.
“Kila familia yenye yenye sifa na hadhi ya umasikini itafikiwa na hakuna Mtanzania mwenye hadhi na sifa ya kunufaika na ruzuku ya TASAF atakayeachwa nyuma,watafikiwa wote ili waondokane na umasikini ambapo zaidi ya sh. trilioni 2.3 zimetengwa na serikali ya awamu ya sita kwa ajili hiyo,”alisema Mchengerwa.
Alisema kuelekea uchumi wa juu dhamira ya serikali ni kuwawezesha wananchi wote wenye hali ngumu ya maisha wapate uwezo wa kumudu gharama za maisha, hivyo hakuna kaya yenye sifa itakosa fedha za TASAF ambapo Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza atawashika mikono.
Waziri huyo wa Utumishi na Utawala Bora,alisema ni jukumu la Mfuko huo wa Mandeleo ya Jamii (TASAF) kuhakikisha wanawawezesha watoto wa familia masikini wanaosoma kwa ngazi ya sekondari na vyuo vikuu watimie ndoto zao hasa watoto wa kike ili hatimaye wawakomboe wazazi wao.
Mchengerwa aliwaondoa hofu wanaufaika kote nchini wasinyong’onyee kwa sababu ya umasikini na kuhoji kwa nini watoto wao wasisome ilhali serikali ya awamu ya sita imesema wasome bure waje kuwakomboa na kuahidi itawasimamia watakaofanya vizuri wapate mikopo ya elimu na ajira baada ya kuhitimu.
“Watoto wa wanufaika wa fedha mfuko wa TASAF ni miongoni mwa wanaopaswa kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo,tutawasimamia waipate ikiwemo ajira,pia tuko kwenye uchumi wa kati tunapaswa kwenda uchumi wa juu,haiwezekani wachache wabaki,lazima twende wote hivyo wanufaika wa fedha hizo wazitumie vizuri kujikomboa kiuchumi na umasikini wa kipato,”alisema.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amina Makilagi,alisema kiasi cha sh. bilioni 61 kilitolewa mkoani humu kwa walengwa zaidi ya 58,000 na kati ya hizo sh. bilioni 32 ziliwanufaisha wananchi wa Wilaya ya Misungwi,ingawa bado zipo kaya zinakabiliwa na umasikini mkubwa.
“Dhamira ya serikali kuwakomboa wote wanaokabiliwa na hali duni ya maisha na fedha hizo ni ukombozi kwa wananchi wetu,wote watafikiwa na hakuna mtu atabaki,pia tuinashukuru kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo cha afya Nyang’homango kutokana na tozo za miamala ya simu,pia miradi ya kimkakati inaendelea hakuna utakaosimama, ”alisema.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyang’homango, Richard Mujalifu, alisema kaya 269 zilitambuliwa na zenye sifa zinazonufaika ni 218, pia miradi miwili ya ajira za muda za uchimbaji wa visima na bwawa la maji iliyogharimu zaidi ya sh. milioni 12.6 iliibuliwa na wananchi mwaka 2017/18.
Naye Diwani wa Kata ya Usagara Mwenyekiti wa Hlamashauri ya Misungwi,Kashinde Machibya, aliishukuru Serikali na Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, kuziwezesha kaya masikini kiuchumi lakini pia kuwaletea fedha za ujenzi wa kituo cha afya ambacho kimetoa jibu la wapi wananchi wakiwemo wanufaika wa TASAF watapata huduma za matibabu.
Katika hatua nyingine Mchengerwa alisema serikali imesikia kilio cha wananchi wa Usagara na Misungwi kuhusu kero ya maji na kuahidi kuishughulikia kabla ya mwaka 2025.
Pia itaongeza sh. milioni 500 za ujenzi wa kituo cha afya cha kisasa, vifaa tiba na dawa ili kuwasogezea karibu huduma za matibabu akina na mama na watoto wachanga na kuwanusuru na vifo vinavyoepukika.
Aidha Mchengerwa alimkatia Bima ya Afya (NHIF) mtoto mwenye ulemavu wa miguu,Alfa William (8) ambaye ni mtoto wa mmoja wa wanufaika wa TASAF kwa ajili ya matibabu na kumwezesha kufanyiwa upasuaji wa viungo vyake na huduma nyingine za afya