SERIKALI imeagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kote nchini, kuchunguza na kuwahoji viongozi wa serikali za vijiji,mitaa na vitongoji wanaodaiwa kuingiza watu wasio na sifa kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini kupitia TASAF.
Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Nyamatongo na Katunguru, wilayani Sengerema, baada ya malalamiko kuwa baadhi ya kaya zenye vigezo na sifa hazikuingizwa kwenye mpango wa TASAF.
Aliiagiza TAKUKURU kuchunguza madai kuwa watu wasio na vigezo na sifa za kunufaika waliingizwa kwenye mpango wa TASAF Awamu ya III kipindi cha II na kuachwa wenye vigezo na kisha kuwachukulia hatua wahusika wote.
“Rais Samia Suluhu Hassan, amenituma kuwaletea salamu zake,miradi ya TASAF ni yake na awamu ya tatu hii ni tofauti na awamu zilizopita.Hapa Nyamatongo na Katunguru,TASAF mmetuangusha mmeacha watu wenye sifa mkaweka watu wenu,nawaagiza TAKUKURU nchi nzima chunguzeni na kuwahoji wahusika wote,tujiridhishe kama wenye sifa wameachwa,”alisema Mchengerwa.
Alisema si malengo ya serikali ya awamu ya sita kuingiza kwenye mpango watu wasio na sifa wakaachwa wenye sifa,walioingizwa kwa ujanja ujanja pamoja na viongozi waliohusika wote wakamatwe kama kuna jinai,pia TAKUKURU ichunguze madai ya baadhi ya watu kupunjwa na kulipwa kidogo na wengine kikubwa,hatataka kusikia hilo.
Waziri huyo wa Utumishi na Utawala Bora alisema Rais Samia, ametoa fedha kwa dhamira ya kuwakomboa Watanzania wanyonge na kuhakikisha kaya zote nchini masikini zinashikwa mkono,kama kuna vijiji havikufikiwa TASAF warudi kufanya tathmini na kupitia upya wapate takwimu sahihi ili waliosahaulika ama kuachwa nao wanufaike.
“Sitegemei watendaji wangu wa chini kunikwamisha na kuchomeka watu wasio an sifa, kama kuna mapungufu yaboreshwe ama watendaji wabadilishwe na hatua zichukuliwe kwa waliohusika,”alisema Mchengerwa na kuahidi kutoa sh. bilioni 130 kwa mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera na wananchi wa Nyamatongo ataangalia awafanyie nini kwani fedha hizo anazo tayari.
Awali Diwani wa Kata ya Nyamatongo (CCM), Yanga Makaga, alimweleza Mchengerwa kuwa, Kijiji cah Karumo wapo wanufaika 59 ambapo mmoja hajawahi kupokea fedha za TASAF,kwamba akitibu ugonjwa huo atalala usingizi kwani kaya zilizoachwa kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini ni kura zisizo na chenga kuliko vijana na kuomba zitambuliwe zipate stahiki zao.
Naye Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu, alisema kuna shida, kwamba Kazi Iendelee wananchi wanaikubali lakini haitaendelea kwa madai wanufaika wa TASAF hawapajata fedha zao,baadhi wameachwa na yawezekana ni hujuma inafanyika kumkwamisha Rais Samia Suluhu Hassan,na ipo mipango inahatarisha usalama wa nchi kwenye huduma za wananchi.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amina Makilagi,alisema mwenye kuwatambua walengwa wa TASAF ni mwenyekiti wa kijiji,yawezekana baadhi walikuwa hawajafikiwa kwa vigezo,hivyo watendaji warudi kuwatambua na kuwaingiza kwenye mpango kwani Rais Samia hataki kusikia ameachwa mtu baada ya utambuzi.
Alisema serikali iliweka utaratibu kwa kaya zinanonufika na TASAF kupokea fedha kwa njia ya mtandao wa miamala ya simu na benki ili kurahisha upokeaji wa fedha nchi nzima,kama zipo changamoto za mfumo zitaangaliwa na kurekebishwa ili kwenda mbele zaidi,pia wanufaika wadhibiti simu zao kuepuka kuibiwa fedha.