Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwasili Kibaha kukagua ujenzi wa Jengo la CCM Mkoa wa Pwani. Oktoba 7,2021.
Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea maelezo kutoka kwa fundi anayehusika katika ujenzi wa Jengo la CCM Mkoa wa Pwani wakati alipofika kukagua ujenzi huo. Oktoba 7,2021.
Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea maelezo kutoka kwa mwenyekiti wa CCM Pwani Ramadhan Maneno juu ya maendeleo ya ujenzi wa Jengo la CCM Mkoa wa Pwani. Oktoba 7,2021
*******************************
Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango Oktoba 7, amekagua ujenzi wa jengo la CCM Mkoa wa Pwani linalotarajiwa kutumika kama chanzo cha mapato ya Chama mkoani humo.
Makamu wa Rais ameagiza kufanyika kwa tathimini ya kina ya ujenzi wa jengo hilo na kupata gharama halisi za ujenzi, kufahamu fedha zilizotumika mpaka sasa ili kuepusha upotevu wa vifaa vya ujenzi na fedha kutokana na kukosekana taarifa sahihi za ujenzi. Aidha Makamu wa Rais ameahidi kuchangia mifuko mia tano ya saruji baada ya kupokea taarifa yenye tathimini sahihi ya ujenzi wa jengo hilo.
Kuhusu migogoro ya ardhi, Makamu wa Rais na mlezi wa CCM Pwani Dkt. Philip Mpango amewataka viongozi wa CCM kukomesha vitendo vya dhuluma na uporaji ardhi za wananchi mara moja ili kuondoa migogoro ya ardhi iliopo mkoani Pwani. Aidha ameagiza serikali ya mkoa kwa kutumia vyombo husika kufanya uchunguzi wa kina na haki na wahusika wote wanaosababisha migogoro ya ardhi hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Makamu wa Rais amekemea uhujumu wa miundombinu katika miradi ya kimkakati kama vile Reli ya Kisasa ya Mwendokasi (SGR) unaofanywa na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Pwani. Amewasihi wanachama wa CCM mkoa wa Pwani kusimamia maadili ya Chama na kupiga vita rushwa na uonevu katika jamii.
Aidha amewataka vijana wa mkoa wa Pwani kutumia fursa ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali mkoani humo kujiinua kiuchumi. Amesema idadi ya vijana wa mkoa wa Pwani katika miradi mbalimbali mkoani humo ni ndogo hivyo hawana budi kuchangamkia fursa hizo.
Makamu wa Rais na Mlezi wa CCM mkoa wa Pwani amewaagiza wabunge na madiwani wa mkoa huo kushirikiana katika kuwaletea wananchi maendeleo ikiwa pamoja na kufanya ziara kwa pamoja na kusimamia utekelezaji wa ilani ya Chama ya mwaka 2020.
Amewaagiza wananchi wa mkoa wa Pwani kujiepusha na vitendo vyote vya uharibifu wa mazingira ikiwa pamoja na kuhakikisha wanafuata kanuni bora za kilimo na uvunaji miti. Amesema athari za uharibifu wa mazingira ni kubwa hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuzuia uharibifu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.
Awali mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno ameishukuru serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Pwani kupitia tozo hasa katika elimu na afya pamoja na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa mradi wa umeme katika Bwawa la Mwalimu Nyerere pamoja na ujenzi wa Reli ya kisasa ya Mwendokasi (SGR).
Makamu wa Rais na Mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani Dkt. Philip Mpango amehitimisha ziara yake ya chama ya siku mbili mkoani Pwani.