*******************************
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo A. Mathew alipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL Corporation kwa kuendelea kutoa huduma bora za mawasiliano zenye kuleta tija kwa wananchi na Taasisi mbalimbali nchini.
Naibu Waziri ameyasema hayo alipotembelea Banda la TTC Corporation katika Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yaliyoanza leo Oktoba 06 na kutarajiwa kuitimishwa Oktoba 08, 2021 katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.
“Serikali tunataka kuona Shirika linaendelea kuongeza juhudi katika kuwatumikia watanzania kwa kutoa huduma bora zenye ushindani katika soko” amesema Mhe. Mhandisi Kundo.
Katika Maadhimisho hayo, Meneja TTCL Dodoma, Bw. Samson Marwa amesema Shirika limeendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuimarisha huduma za mawasiliano nchini.
“hivi sasa tunaendelea kukamilisha mradi wa kupeleka mawasiliano vijijini na maeneo ya mipakani ambapo kulikuwa na changamoto za mawasiliano, hizi juhudi tunazofanya katika kuhakikisha malengo ya serikali ya kupeleka huduma za mawasiliano zinafanikiwa” amesema Bw. Samson Marwa.
Meneja wa TTCL Dodoma ameongeza kuwa Shirika linatumia Maadhimisho haya kuwakaribisha watanzania wote kutembelea Banda letu ili waweze kupata huduma mbalimbali za simu za mkononi, Simu za Mezani, Huduma za Intaneti kupitia Waya(Fixed broadband) na huduma kwa ajili ya Taasisi na Mashirika.
“Shirika kwa kipindi hiki cha Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani tunahamasisha matumizi ya simu za mezani kwa wakazi wa jiji la Dodoma kwa wale wa majumbani na maofisini, huduma hii ni salama na ya uhakika inayopatikana kwa bei nafuu sana” amesema Bw. Samson Marwa.