Mratibu wa Semina juu ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa kutoka GST Gabriel Mbogoni akizungumza na vyombo vya habari mapema baada ya kumaliza semina kwa maafisa wa Jeshi la Polisi Dodoma.
*****************************
Na.Samwel Mtuwa – GST.
Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma limeipongeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kutoa elimu juu ya kujikinga na Majanga ya asili kwa maafisa mbalimbali wa Jeshi hilo walioudhuria semina hiyo iliyofanyika leo Oktaba 7, 2021 katika Ukumbi wa Polisi.
Akizungumza wakati wa kufungua semina hiyo Kamishna Msaidizi wa Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma katika kitengo maalum cha Operesheni ya kushughulika na Majanga ya asili Edward Balele ameipongeza GST kupitia wataalam wake kwa kulishirikisha Jeshi la Polisi katika kupambana na Majanga ya asili yanayotokea nchini.
Akizungumzia juu ya majukumu ya Jeshi hilo , Kamishna Balele alifafanua kuwa Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda Raia na Mali zake hivyo ni muhimu sana kupata ufahamu juu ya Majanga ya asili ya Jiolojia ili pindi yanapotokea wawe na uelewa mzuri wa namna bora ya kuokoa jamii na Mali zake bila kudhurika na janga hilo.
Kwa upande wa Mratibu wa semina hiyo kutoka GST Gabriel Mbogoni aliwaeleza maafisa wa Polisi kuwa Majanga ya asili hayatabiriki hivyo ni ngumu kuyazuia , kutokana na hali hiyo wataalam wa GST wameamua kutoa elimu kwenu itakayosaidia Kupunguza maafa pindi yatakapotokea, pia GST inaamini kuwa kutoa elimu hii kwenu itakua njia nzuri kwenu kutoa kwa wengine ambao hawajapata fursa ya kuhudhuria leo.
Kupitia Maudhui ya siku ya Kimataifa ya kupunguza Maafa , GST itaendelea kutoa elimu kwa Umma juu ya kujikinga na Majanga ya asili kama vile maporomoko ya Ardhi , Matetemeko ya Ardhi , Mipasuko ya Ardhi na Majanga mengine yenye asili ya kijiolojia.