…………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt .Philip Isdor Mpango ameshtushwa kupata fununu ya baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, kuhusika kuwa vinara wa kuchochea wananchi kuhujumu miundombinu ya miradi ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa (SGR) pamoja na kupora ardhi za wanyonge.
Aidha ameziagiza kamati za siasa kuanza kubaini kambi na makundi ambayo yameanza kujitokeza kuanza kampeni za chinichini kuelekea katika uchaguzi wa ndani wa CCM mwaka 2022.
Pamoja na hilo ,Mpango amehimiza, wananchi kujitokeza katika zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani .
Akizungumza na madiwani,wabunge na kamati za siasa Wilaya na mkoa mkoani Pwani ,alisema pamoja na mafanikio yaliyopo Pwani amebaini changamoto sita ambazo zinahitaji ufumbuzi ili kupata ushindi mzuri uchaguzi mkuu ujao 2025.
Mpango alieleza ,kubwa ni kuhujumu miradi ya kitaifa ya kimkakati ikiwemo mradi mkubwa wa umeme (Stigo )Rufiji na reli ya kisasa (SGR) ambapo baadhi ya wananchi wakichochewa na viongozi wa CCM .
“Upo wizi wa saruji pale mradi wa umeme Rufiji na kwenda kuuza Kwingine vitendo hivi havikubaliki na havivumiliki “
Pamoja na hilo, kusheheni kwa migogoro ya ardhi inayohusisha baadhi ya viongozi wa CCM na watumishi wa ardhi kupora maeneo.
“Nimesikitishwa kusikia wapo wanaohusika kupokonya haki za wanyonge,naagiza hili lisimamiwe na likomeshwe ibaki historia “
Mpango aliipongeza Mkuu wa mkoa wa Pwani, Aboubakari Kunenge kwa kusimamia changamoto hizo na kukaza kamba kwa hayo ,hivyo ameviagiza vyombo vya dola na taasisi husika kupeana taarifa linapotokea tukio na kuimarisha ulinzi wa miundombinu.
“Miradi hii inatekelezwa kwa jasho la watanzania kwahiyo vyombo vya dola viimarishe ulinzi na kuchukua hatua kali za kisheria pale wanapobaini wahusika”
“WanaCCM mzingatie msingi wa maadili,ibara ya 113-116 ya ilani ya utekelezaji ya CCM imeweka msisitizo wa kupambana na rushwa ,Msiwe sehemu ya hii dhuluma ,tutanyimwa kura “alifafanua Mpango.
Akitaja changamoto nyingine ni za kiuchumi ,amewataka kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuagiza miradi na raslimali iliyopo kuilinda .
Katika hili aliagiza kuona thamani ya fedha kwenye ujenzi wa jengo la CCM mkoa ambalo limechukua muda mrefu na mjenzi kutimiza kazi yake.
Mpango alitaja na changamoto ya kadi za kielektroniki na ametoa hofu kuwa hatua zinachukuliwa na wakati wowote tatizo hili linakwisha.
Akizungumza kuhusiana na fursa za vijana Pwani ,ili kujiimarisha kiuchumi alitoa rai kwa vijana kuchangamkia fursa zilizopo ukizingatia mkoa huo una viwanda vingi .
Wakati huo huo ,Mpango alipongeza kumalizwa kwa mvutano ndani ya kamati ya siasa mkoani Pwani na kudai hataki na hatopenda kusikia moshi unafukuta Tena .
Aliwasihi madiwani na wabunge kushirikiana na kuagiza wabunge na madiwani ratiba zao za ziara kuhakikisha wanapelekea nakala kamati ya siasa na mkoa.
Mpango hakusita kupokea changamoto zilizotolewa na Mwenyekiti wa CCM Pwani Ramadhani Maneno kuhusu kufungua baadhi ya barabara muhimu ikiwemo Mkuranga, Rufiji-
Mloka ,Makofia- Mlandizi na kutatua tatizo la Bandari ya Bagamoyo.
Awali Maneno aliipongeza serikali kwa hatua ilipofikia mradi wa daraja jipya la kisasa WAMI ambalo linakwenda kufungua milango ya kiuchumi.
Maneno aliipongeza Serikali kwa utekelezaji wa ilani hasa kwenye miradi ya kimkakati na fedha zilizotokana na miamala ya tozo kutumika vizuri na faida yake kuonekana .
Nae MNEC Pwani,Hajji Jumaa aliishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kupunguza wigo wa kundi la wenye ulemavu kukopesheka kutoka watano hadi mmoja ambae anaweza kukopesheka kupitia asilimia 10 kwenye Halmashauri.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Aboubakari Kunenge alisema wamepokea maagizo yote na watayafanyia kazi .
Alisema dhamana waliyopewa ni kutumikia wananchi na kuiahidi serikali kutoiangusha.