*********************************
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
UONGOZI wa Zahanati ya Nala umetakiwa kujipanga kuwatembelea wananchi katika maeneo yao na kuwaelimisha ili waweze kuchanja chanjo dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Muuguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Situ Muhunzi alipoongoza timu ya wataalam wa Afya wa Jiji la Dodoma kutembelea Zahanati ya Nala jijini Dodoma.
Muhunzi alisema kuwa uongozi wa zahanati hiyo unatakiwa kujipanga vizuri na kuwafuata wananchi katika maeneo yao kuwaelimisha juu ya chanjo ya dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19 ili wafanye maamuzi baada ya kuwa na elimu ya kutosha. “Niwashauri kutoka na kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kuwaelimisha. Wale watakao kubali kuchanjwa kwa hiari wachanjwe hukohuko katika maeneo yao. Utaratibu huu ni mzuri kwa sababu utawaondolea adha wananchi ya kufuata chanjo kituoni hapa” alisema Muhunzi.