Dkt. Revocatus Balterzary akiongea na wananchi wa Mtaa wa Kawawa jijini Dodoma
……………………………………………………………….
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wa Mtaa wa Kawawa katika Kata ya Mbalawala wameshauriwa kuchanja chanjo dhidi ya ugonjwa wa uviko-19 unaosababishwa na virusi vya corona ili kuepuka vifo.
Kauli hiyo ilitolewa na mtaalam kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Revocatus Baltazary alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa wa Kawawa uliopo Kata ya Mbalawala kwenye mkutano wa hadhara wa mtaa.
Dkt. Baltazary alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kama yalivyo maeneo mengine imeathirika na ugonjwa wa Uviko-19. “Bahati nzuri kwa sasa tuna chanjo dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19. Tunashauri wananchi tupate chanjo hiyo. Chanjo hiyo ni hiari na haina madhara yoyote. Mwenyekiti wa Mtaa umechanja jana, je umepata madhara gani baada ya kuchanja? (Mwenyekiti alijibu hapana, kwa ujasiri). Wananchi wanapochanja wengi, tunazuia maambukizi na kuenea kwa ugonjwa huo katika jamii” alisema Dkt. Baltazary.