Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio kuhusu maandalizi ya ujenzi wa mradi wa LNG ( mradi wa kusindika gesi kuwa kimiminika ) katika eneo Likong’o Manispaa ya Lindi wakati alipotembelea eneo hilo akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Lindi, Oktoba 5, 2021. Kulia ni Mkuu wa Mkoa a Lindi, Hajat Zainab Telack.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio kuhusu maandalizi ya ujenzi wa mradi wa LNG ( mradi wa kusindika gesi kuwa kimiminika ) katika eneo la Likong’o Manispaa ya Lindi wakati alipotembelea eneo hilo akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Lindi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama michoro ya ujenzi wa mradi wa maji wa Mitwero, Mkwaya na Kitunda wilayani Lindi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mnara iliyopo Rondo katika Jimbo la Mtama Mkoani Lindi
Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Benard Membe (katikati), Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Lindi, Athumani Seif (kulia) na Mkuu wa wilaya Mstaafu, Naaz Mangochi wakifurahia hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mnara katika jimbo la Mtama, mkoa wa Lindi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Bruno Ngonyani wakati alipotembelea hospitali ya Nyangao katika Jimbo la Mtama, Oktoba 5, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kwa dhati kuhakikisha kuwa mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) utakaogharimu Dola za Kimarekani bilioni 30 sawa na takriban shilingi trilioni 70, unaanza kazi ili kuleta manufaa kwa wananchi.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 5, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Likong’o wilayani Lindi baada ya kukagua eneo la ujenzi wa mradi wa LNG akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa wa Lindi.
Amesema kwa sasa mradi huo umefikia katika hatua ya majadiliano ya kimkataba na wawekezaji wa mradi huo, hivyo amewataka waliochukua viwanja karibu na eneo la mradi waanzeni kuvijenga kwani baada ya kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na watu wengi watakaohitaji makazi.
“Mradi huu unakuja na fursa nyingi za kimaendeleo, zikiwemo ajira kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka eneo la mradi pamoja na Watanzania kwa ujumla hivyo tujitahidi kuwa walinzi wa eneo hili lisivamiwe. Mheshimiwa Rais Samia amepania kuutekeleza katika awamu hii ya sita.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio amesema wakazi zaidi 600 wa mitaa ya Likong’o na Mto Mkavu katika Manispaa ya Lindi wameshalipwa shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya kupisha mradi wa LNG. Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 2071.
Dkt. Mataragio amesema Oktoba 20 mwaka huu Serikali ya Tanzania kupitia TPDC inatarajia kufanya majadiliano na wawekezaji kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo. Aliongeza kuwa kwa sasa waendelea na uwekaji wa alama zinazoonekana kuzunguka eneo lote la mradi ili liweze kutambuliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo nchini, hivyo amewataka wananchi wafanye maandalizi ya kufikisha nishati hiyo katika makazi yao.
Alisema Mheshimiwa Rais Samia anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme nchi nzima ikiwemo na vijiji vya wilaya ya Lindi. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.
Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nyaya, nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali.