Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akikabidhiwa nakala za vitabu vya “Uchumi wa Bluu” na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dk. Tumaini Shaban, ambaye ni mwandishi wa kitabu hicho wakati alipotembelea Chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam, Dkt. Erick Massami, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, wakati alipotembelea na kukagua utendaji kazi wa chuo hicho kilichopo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Kutoa Huduma za Ukarabati wa Vyombo vya Kuokolea Maisha kutoka Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam (DMI), Mhandisi Victor Eucharius Kilindo, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, namna ya kujiokoa ndani ya boya maalum ukiwa umekwama baharini.
Mkuu wa Kitengo cha Karakana kutoka Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam (DMI), Mhandisi Ibrahim Mpapi, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, wakati alipotembelea na kukagua utendaji kazi wa chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………….
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ametoa wito kwa vijana kusoma mafunzo ya ubaharia ili kuunga mkono juhudi za Serikali kufikia malengo yake, hususan ya kupanua wigo wa ajira kupitia kazi za kitaaluma na umahiri.
Hayo yamezungumzwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri huyo katika ziara yake ya kikazi katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).
Waitara amesema kuwa chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1978 kimepata mafanikio makubwa ya kuwepo kwenye orodha ya vyuo bora vya Shirika la Bahari Duniani tangu mwaka 2003 na hivyo kufanya wanafunzi wanaofuzu mafunzo katika chuo hicho kupata fursa za ajira kwa nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Uganda, Visiwa vya Comoro, Namibia, Burundi, Ugiriki, Singapo na nchi za Falme za Kiarabu na Mashariki ya Kati.
“Nimepata sifa nzuri za wanafunzi waliomaliza kwenye chuo hiki na kwamba elimu inayotolewa hapa ni ya kimataifa na chuo kinaongoza kwa kutoa fursa nyingi za ajira na kutoa mchango mkubwa kwa Taifa”, amesema Naibu Waziri Waitara.
Aidha, Waitara amesema Serikali itaendelea kukiwezesha chuo hicho kwa kuwekeza fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na ukarabati wa miundombinu ya karakana ya chuo hicho ili kuendelea kuzalisha wataalam wengi zaidi na wenye sifa.
“Tunahitaji chuo hiki kiongeze vifaa na kiendelee kukubalika kwa viwango vya kimataifa kwa kutoa elimu na mafunzo ya nadharia na vitendo kwa ufasaha ili kutimiza azma ya Serikali katika kuendeleza uchumi wa bluu hivyo changamoto zenu zimefika na zitafanyiwa kazi”, amesisitiza Waitara.
Amefafanua kuwa taasisi hiyo ni muhimu kwa nchi yetu ambapo kwa sasa imeendelea kutambulika nchi jirani za Kenya, Malawi, Namibia, Zambia, DRC, Uganda, Rwanda, Burundi, Eritrea na Comoro ambapo raia wake wamekuwa wakitumia chuo hicho kupata mafunzo mbalimbali katika sekta ya bahari na ubaharia.
Naibu Waziri Waitara amewataka wakufunzi na watumishi kutumia vizuri nafasi ya uwepo wao chuoni hapo kwa kuzalisha wataalam wanaokidhi mahitaji ya soko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha DMI, Dkt. Erick Massami, amemueleza kuwa chuo hicho kimepanga kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 7.8 kwa mwaka huu wa fedha wa 2021/22 ambapo mpaka sasa chuo kimefanikiwa kudahili jumla ya wanafunzi 3,237 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,283 kutoka 1,954 kwa mwaka uliopita 2019/20.
Dkt. Massami amemueleza Naibu Waziri huyo licha ya mafanikio ya chuo wanayoyapata na kutambulika kimataifa, chuo bado kina ukosefu wa mabweni kwa wanafunzi hasa wale wa vyeti na diploma ambao badi ni wadogo na wahitaji usimamizi pamoja na upungufu wa madarasa ya kufundishia wanafunzi hao.
Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam ni moja ya taasisi zilizopo chini ya usimamizi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ambacho kimejikita zaidi kwenye utoaji wa elimu katika sekta ya usafiri wa majini.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi