Mshambuliaji Bakari Nyungure (mwenye mpira) wa timu ya soka ya Uchukuzi akiwahi mpira katika mazoezi ya timu hiyo inayojiandaa na michuano ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI, itakayofanyika jijini Morogoro kuanzia Oktoba 20 hadi Nov 2, 2021.
Baadhi ya wachezaji wa klabu ya Uchukuzi wa michezo mbalimbali wakimsikiliza Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alphonce Mwingira (hayupo pichani ) wakati akiongea nao baada ya mazoezi ya kujiandaa na michuano ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), itakayoanza Oktoba 20 hadi Novemba 2, 2021 mkoani Morogoro.
Mwenyekiti Alphonce Mwingira (aliyenyoosha mkono) akiwa na viongozi wenzake wa klabu ya Uchukuzi wakati wakiongea na wachezaji wa michezo mbalimbali wakijiandaa na michuano ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), iliyopangwa kufanyika jijini Morogoro kuanzia Oktoba 20 hadi Novemba 2, 2021.
Wacheaji wa timu ya wanawake ya kuvuta kamba ya klabu ya Uchukuzi wakifanya mazoezi ya kujiandaa na michuano ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), itakayoanza Oktoba 20 hadi Novemba 2, 2021 mkoani Morogoro.
*********************************
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Klabu ya Michezo ya Uchukuzi, Alphonce Mwingira amewasha moto wa kutwaa ushindi wa vikombe vya michezo mbalimbali itakayoshindaniwa kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali nchini (SHIMIWI), iliyopangwa kuanza tarehe 20 Oktoba, 2021 hadi tarehe 2 Novemba mkoani Morogoro.
.
Mwingira amewasha moto huo hivi karibuni alipotembelea mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye viwanja vya Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), maeneo ya Banana, Ukonga, ambapo amewatia moyo na ari wachezaji kwa kuwataka kuendeleza wimbi la ushindi.
Amesema sifa ya klabu hiyo ni kutwaa ubingwa wa michezo mbalimbali, ikiwemo kutwaa ubingwa wa jumla, hivyo anatarajia ushindi huo kuendelezwa ili kuiletea sifa Sekta ya Uchukuzi.
“Najua kuwa sisi ni kawaida yetu kushinda kwenye mashindano mbalimbali, na CV yetu ni kubwa hivyo tusiichafue hivyo ule moto mliokuwa mkiuwasha kule kwenye mashindano ya Kombe la Mei Mosi tulikuwa tunauona na kuufuatilia mkauendeleze huko Morogoro na mrudi na ushindi kwa michezo yote na wizara ipo pamoja na nyie kwa hali na mali,” amesema Mwingira.
Hatahivyo, amewahimiza wachezaji kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, na atakayekiuka atachukuliwa hatua za kinidhamu kulingana na taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma, baada ya taarifa kuwasilishwa kwa Mkuu wake wa taasisi na Idara.
Awali Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Hassan Mohamed amewataka wachezaji kutambua wanacheza kwenye timu yenye jina kubwa na inayoundwa na wachezaji waliowahi pia kucheza ligi kuu Tanzania Bara na pia kuwania uraisi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Ally Tembele; na kuwa na viongozi wa juu wa chama cha netiboli nchini (CHANETA), Judith Ilunda, ambaye ni Katibu na Hilda Mwakatobe ni mjumbe.
“Wapo wengine kama watatu ni viongozi kwenye SHIMIWI kama Naibu Katibu na Wajumbe katika kamati ndogo ndogo, hivyo timu yetu inamchango mkubwa katika michezo,” amesema Mohamed.
Naye Katibu Mkuu wa timu hiyo, Bura Tenga amewashukuru makocha wa michezo yote kwa kujitoa kwa moyo kufanya maandalizi ya wachezaji kwa ajili ya michuano hiyo inayotarajiwa kuwa na wachezaji Zaidi ya 2000 kutoka kwenye Wizara, Taasisi na Idara za SerIkali.
Kocha Eulitery Mollel ameomba uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha timu zote zinaingia kambini katika angalau kwa wiki mbili, ili kuleta uimara wa kucheza pamoja kutokana na timu hii inaundwa na wachezaji kutoka mikoa mbalimbali.
“Pamoja na kuanza mazoezi wachezaji wa hapa Dar es Salaam pekee, tunawachezaji wengi wa mikoani kulingana na taasisi zetu zinazounda Sekta ya Uchukuzi hivyo, basi hatupo pamoja na tunaweza tusicheze kama timu kutokana na kutokaa pamoja, hivyo ombi langu kwenu tuingie kambini wiki mbili za mwisho kabla ya kwenda kwenye mashindano tuwe pamoja kama timu,” amesema Mollel.
Michezo inayotarajia kushindaniwa kwa kuhusisha timu za wanawake na wanaume ni pamoja na ya kuvuta Kamba, kuendesha baiskeli, riadha kuanzia mita 100, 200, 800 na relay 100×4, draft, bao, karata, wakati michezo ya soka ni wanaume na netiboli ni wanawake