Ligi ya mbunge wa Jimbo la Ulanga mkoani Morogoro inayojulikana kwa jina la SALIM ALMAS CUP imemalizika rasmi kwa kushuhudia timu ya Bodaboda kuwa bingwa kwa upande wa mpira wa miguu na timu ya Vijana Queens kwa upande wa Netiball.
Ligi hiyo ambayo imedumu kwa takribani miezi 6 tangu ilipoanzishwa na ilikusanya jumla ya timu 216 ambazo zilichuana kuanzia ngazi ya kata, tarafa na baadae kupata timu nne zilizoingia fainali ambazo ni Bodaboda na Msewa Academy kwa upande wa mpira wa miguu na Vijana Queens dhidi ya Polisi Jamii kwa upande wa netball.
Fainali hiyo ambayo ilivuta hisia za mashabiki wa wilaya hiyo ya Ulanga imeshuhudia mabingwa hao wakijinyakulia zawadi mbalimbali kwa kila mmoja ambapo kwa upande wa mpira wa miguu bingwa alijinyakulia kiasi cha shilingi milioni moja na nusu,kombe na medali wakati mshindi wa pili akijinyakulia kiasi cha shilingi milioni moja na medali na mshindi wa tatu akijinyakulia laki tano pekee na kwa upande wa Netball bingwa alijinyakulia kiasi cha milioni moja,kombe na medali wakati mshindi wa pili amejinyakulia laki tano na seti moja ya jezi mpya kabisa.
Baada ya kukabidhi zawadi hizo mbunge wa jimbo la ulanga mhe. Salim Alaudin Hasham Almas amezipongeza timu zote zilizoshiriki ligi na zaidi kuzipongeza timu mbili mabingwa ambazo ni Bodaboda na Vijana Queens kwa kuibuka na ubingwa huo ikiwa ni msimu wa kwanza wa ligi hiyo.
Aidha Almas amewataka vijana wote walioshiriki katika ligi hiyo kuendeleza vipaji vyao kwani fursa ni nyingi katika michezo na kwa hivi sasa michezo hutumika kama fursa za ajira na amewaahidi kuwasaidia kwa wale watakaohitaji msaada wa kusogea zaidi ili kupata wachezaji wengi kutoka jimbo hilo.
Pia Almas ameahidi kuchagua vijana 10 kwa upande wa mpira wa miguu na netball ili awasaidie kupata timu zinazoshiriki ligi kubwa na waendeleze vipaji vyao.
Almas pia ameahidi kuchagua timu mbili ya wanawake kwa Netball na wanaume kwa Mpira wa miguu ambazo zitapata fursa ya kucheza mechi za kirafiki katika mkoa wa dodoma na timu zinazoshiriki ligi kuu na ligi daraja la kwanza ili kujiongezea uzoefu zaidi.
Huu ni msimu wa kwanza wa ligi hiyo ya mbunge Salim Almas Cup na ameahidi kufanya hivyo kila mwaka mpaka pale atakapopata timu itayowakilisha jimbo hilo katika ligi za juu ikiwemo ligi kuu.