***********************************
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WALIMU wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni watu muhimu katika kutoa elimu na uhamasishaji kwa jamii ili iweze kufanya maamuzi sahihi katika kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na maelfu ya walimu wa Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Shekimweri alisema kuwa uongozi wa wilaya umeamua kukutana na kutoa elimu kwa kundi la walimu kutokana na umuhimu wao katika jamii. “Sote tunafahamu kuwa dunia imepata tatizo la ugonjwa wa Uviko-19 unaosababishwa na virusi vya Corona. Walimu hawajapewa msamaha kupata ugonjwa huu. Tulifikiri kama viongozi wa wilaya tupate muda wa kutafakari pamoja. Tunafahamu kuwa kuna kundi la walimu waliopata ugonjwa huu. Tahadhari zinachukuliwa ila bado kuna maambukizi na vifo” alisema Shekimweri.
Alisema kuwa mwalimu akipoteza maisha ni hasara kwa familia yake na taifa kwa ujumla. “Ndugu zangu, ukiangalia kundi linalokutegemea na dhamana yako kwa jamii na darasa lako unalolipenda una wajibu wa kufanya maamuzi sahihi. Kila mmoja atafakari na kuchukua hatua kwa hekima. Uviko-19 ni jambo la kufa na kupona, tusichukulie kwa mzaha” alisisitiza Shekimweri.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa walimu ni kundi muhimu sana katika kuelimisha jamii ili ifanye maamuzi sahihi. “Walimu mkielewa vizuri suala la chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19, mnaweza kuelimisha bodi na kamati za shule” alisema Shekimweri.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa ugonjwa wa Uviko-19 upo katika Jiji la Dodoma na njia za kukabiliana nao ni kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa na kuachiana nafasi. “Ndugu zangu pamoja na njia hizo, tunayo chanjo ya ugonjwa huo. Tumeshuhudia ndugu zetu wakiugua ugonjwa huu na kufariki. Tumeshuhudia vifo vya watumishi na marafiki zetu. Kuna vifo vya watumishi wa Afya vilivyotokana na wao kuwahudumia wagonjwa wa Uviko-19. Tumeshuhudia vifo vingi vya walimu wetu kutokana na kutekeleza majukumu yao” alisema Dkt. Method kwa uchungu.