Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) nchini, Dkt.Suleiman Muttani, akizungumza kwenye kikao kilicho wakutanisha wadau mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kujadili mbinu bora za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Baadhi ya wadau wakiwa kwenye kikao hicho.
Picha ya pamoja.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) kupitia mradi wa ‘AWARE 2020’ limewakutanisha wadau mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa ajili ya kujadili na kupata ufumbuzi na mbinu bora za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Wadau waliokutanishwa na shirika hilo katika kikao hicho ni Kamati za Vijiji za Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), Majukwaa ya vikundi vya Sauti ya Mwanamke, Sauti ya Wanafunzi na Jukwaa la Wanaume Washawishi ambao wanapinga vitendo vya ukatili (kama ubakaji, ulawiti, ukeketaji, ndoa za utotoni) , vipigo kwa wanawake na ukatili kwa watoto katika vijiji vinne vya mradi ndani ya wilaya hiyo.
Vijiji hivyo vya mradi ni Siuyu na Unyankhanya vilivyopo Kata ya Siuyu, Munkinya na Damankia kutoka Kata ya Dung’unyi.
Kikao hicho cha wadau kilichofanyika mwishoni mwa wiki wilayani humo kililenga kufanya majadiliano ili kupata ufumbuzi na mbinu bora za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambao umekithiri mkoani hapa.
Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF nchini, Dkt.Suleiman Muttani alisema shirika hilo chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) limekuwa likitekeleza mradi wa AWARE katika kata 5 za Wilaya ya Ikungi kwa kufanya utetezi wa haki za wanawake na mtoto wa kike dhidi ya athari zitokanazo na mila na desturi kandamizi.
Mshauri wa Masuala ya Sheria wa shirika hilo na Mratibu Msaidizi wa mradi huo , Paul Kigeja alisema lengo la kikao hicho ilikuwa ni kuwakumbusha majukumu yao ya msingi ya kutekeleza kazi zao katika ngazi za vijiji lakini pia kwa pamoja waweze kujadili na kufikia hitimisho la kupata njia bora zaidi za kukomesha vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
“Lakini kwa umuhimu zaidi lengo letu lilikuwa ni namna ya kuweza kuratibu juhudi za pamoja kwani hivi ni vikundi mbalimbali ambavyo vina viongozi wa dini, vijiji, watendaji na kuna baadhi ya kamati zinafanya kazi nzuri lakini hazipati ushirikiano na kamati zingine hivyo tukaona kupitia kikao hiki tuweze kuwakutanisha ili wawe na juhudi na sauti ya pamoja,”.alisema.
Mwanafunzi Gasper Moris kutoka Sekondari ya Munkinya alisema Shirika hilo lina mchango mkubwa kwani limemsaidia kujua mambo mbalimbali ambapo aliweza kumsaidia mwanafunzi mwenye ulemavu aliyekuwa akifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kupigwa na kuchaniwa nguo zake na kuchanjwa chanjwa na wembe.
Mwanafunzi Naina Selemani wa Shule ya Sekondari ya Siuyu ambaye ni kiongozi wa Klabu ya kupinga ukatili shuleni hapo alisema amekuwa akitoa taarifa ya matukio ya ukatili wa kijinsia kwa walimu walezi ambao nao waliyapeleka ngazi za kata jambo lililosaidia kuwafanya wanafunzi kuacha kujihusisha na vitendo hivyo.
Katibu wa Jukwaa la Wanaume Ferdnand Holota ambaye alijiunga na shirika hilo mwaka jana alisema baada ya kupata mafunzo ya kupinga ukatili na wao kwenda kuelimisha jamii sasa na wanaume ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia wameanza kujitokeza hadharani ili wasaidiwe.
“Shirika la SPRF limetuletea mabadiliko makubwa wanaume walikuwa wakiona aibu kujitokeza kuelezea madhira waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa wake zao lakini sasa hivi wanayaeleza na kupatiwa msaada,”alisema Holota.
Mama Marietha Kibao kutoka Sauti ya Mwanamke Kijiji cha Munkinya alisema shirika hilo limeleta mabadiliko makubwa katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuzipa ujasiri kamati za kupinga vitendo hivyo.
“Mambo ya unyanyasaji wa watoto na wanawake vikiwemo vitendo vya ukeketaji mimba za utotoni na ubakaji vimeanza kupungua baada ya mashirika haya kutoa elimu naamini Serikali na wafadhili wengine wakiendelea kuyawezesha vitendo hivi vitakwisha kabisa,”.alisema Kibao.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ikungi, Haroun Yunus Haroun alisema mfumo wa mawasiliano uliopo sasa umesaidia kwa kiwango kikubwa kuwabaini watuhumiwa na kuibua vitendo hivyo vinavyofanyika kwa siri ambapo vimepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na siku za nyuma.