Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwasili katika Ukumbi wa PTA Sabasaba kuzungumza na Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Dar es salaam.Oktoba 5, 2021.
Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Dar es salaam.Oktoba 5, 2021.
Mke wa Makamu wa Rais na Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Mama Mbonimpaye Mpango akipokea zawadi kutoka kwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Dar es salaam Bi. Florence Masunga wakati aliporidhia ombi la kuwa Mlezi wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es salaam.
******************************
Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa Mkoa wa Dar es salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango leo Oktoba 5, 2021 amezungumza na Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Dar es salaam mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa PTA Sabasaba Dar es Salaam.
Dkt. Mpango amewashuruku wanawake wote nchini kupitia UWT kwa kuendelea kuliombea Taifa amani na mshikamano pamoja na kuiombea serikali na viongozi wake. Amesema UWT ni Jumuiya kubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi yenye wanachama wengi hivyo CCM inatambua mchango huo katika ushindi wa chaguzi zake zote.
Aidha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema UWT inapaswa kuwa sauti ya wanawake katika uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kupiga vita ukatili na unyanyasaji wa wanawake katika jamii.
Amesema Mchango unaotolewa na wanawake katika malezi, lishe bora , kulinda maadili katika jamii pamoja na ujenzi wa uchumi ni mkubwa na kuwataka kuendelea kuwa kichocheo cha kujenga Tanzania imara kijamii na kiuchumi.
Aidha Mlezi huyo wa Mkoa wa Dar es salaam amewaasa UWT kufanya juhudi za kuongeza wanachama ,kuhimiza uhai wa wanachama, kufanya vikao vya Jumuiya hiyo, kuwa mstari wa mbele katika ziara za ukaguzi wa uhai wa chama, kulinda Amani ya nchi pamoja na kuepuka migogoro ndani ya Jumuiya hiyo.
Katika hatua nyingine Dkt. Mpango amewasihi UWT kujitokeza pamoja na kuelimisha wananchi kushiriki katika sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022. Amesema ili kupata takwimu sahihi na kupanga mipango ya maendeleo ni muhimu wananchi wote kushiriki katika Sensa hiyo.
Aidha amewaagiza wanawake kuendelea kushiriki katika michezo ikiwa moja ya njia ya kujilinda dhidi ya Uviko 19. Amesema UWT wanapaswa kutoa hamasa ya watu kujitokeza kupata chanjo ya Uviko 19 ili kulinda wananchi wengi katika janga hilo.
Awali akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa CCM Mkoa wa Dar es salaam katibu wa jumuiya hiyo Bi. Grace Haule amesema UWT katika kutimiza miaka 44 tangu kuanzishwa kwake imeshiriki kikamilifu kutoa mchango wake katika ujenzi wa taifa katika sekta mbalimbali kama vile Afya, Elimu, Miundombinu, Nishati, pamoja na huduma ya maji. Aidha ameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha sekta hizo kwani zimekuwa na msaada mkubwa kwa wanawake hapa nchini.
Amesema wanawake mkoa wa Dar es salaam wanatambua juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo hivyo wanaunga mkono juhudi hizo.
Katika Mkutano huo UWT mkoa wa Dar es salaam wamewasilisha ombi kwa mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango kuwa mlezi wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es Salaam ambapo mke wa Makamu wa R ais ameridhia Ombi hilo.