NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
WAFANYABIASHARA katika Mnada wa Ushirika ulipo Mjini Nzega washauriwa kuchangamkia chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 ili waendelee kuwa salama na kuendesha shughuli zao za kujiingizia kipato halali.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati wa ziara yake inayoendelea ya utoaji wa elimu umuhimu wa chanjo ya UVIKO 19 katika maeneo mbalimbali za Mkoa huo.
Alisema afya mtaji muhimu kwa kila mwanadamu na pindi anapokuwa mgonjwa shughuli zake zinateteleka na kurudisha nyuma maendeleo yake.
Balozi Dkt. Batilda Buriani alisema hivyo chanjo ya UVIKO 19 ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameileta ni salama na muhimu katika kulinda afya za wananchi na kuwawezesha kuchapa kazi bila matatizo.
Alisema Rais Samia anawapenda wananchi wake na ndio maana ameamua kuwatafutia chanjo dhidi ya ugonjwa hatari wa UVIKO 19 ambao umeshapoteza nguvu kazi na kuzorotesha uchumi wa dunia.
Balozi Dkt. Batilda alisema kuwa watu waliochanja wako katika mazingira mazuri ya kutopoteza maisha hata kama wakipata maambukizi ya UVIKO 19 , lakini wale ambao hawachanji wako kwenye uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha pindi watakapopatwa na ugonjwa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwaagiza watendaji katika sekta ya Afya kusogeza huduma za chanjo ya kujikinga na UVIKO 19 karibu na maeneo ambayo watu wengi wanaendesha shughuli zao za kujitafutia ridhiki.
Alisema umbali wakati mwingine umechangia baadhi ya wananchi kutoshiriki zoezi hilo la chanjo.
Baadhi ya Wafanyabiashara katika Mnada huo wameishukuru Serikali ya Mkoa wa Tabora kwa kuwapa elimu kuhusu chanjo kwa kuwa hapo awali walikuwa hawana elimu sahihi jambo lililowafanywa kuchelewa kuchanja.
Walisema baada ya kudhibitishwa na Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora kuwa Rais Samia amechanja na viongozi mbalimbali wamechanja na chanjo ni salama wako tayari na kupata chanjo hiyo.