MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Kata ya Makongo, Abiaty Kivea (wa tano kushoto) akikabidhi msaada wa vifaa vya usafi kwa wanafunzi na viongozi wa Shule ya Msingi Changanyikeni, vilivyo tolewa na umoja huo, Dar es Salaam, ikiwa ni kuelekea Kilelele cha Maadhimisho ya Wiki ya UWT kinachofanyika kesho.Watatu kushoto ni Katibu wa umoja huo katika kata hiyo, Deodata Komba.( Na Mpigapicha Wetu).
****************************
Na MWANDISHI WETU
UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT), Kata ya Makongo, umekabidhi vifaa kwaajili ya usafi wa vyoo katika shule mbalimbali za msingi na sekondari katika kata hiyo.
Akikabidhi vifaa hivyo, Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa UWT Kata ya Makongo, Abriat Kivea, amesema ni katika kuadhimisha Wiki ya UWT ambayo inafikia kilele hapo kesho.
“Tuliona tukabidhi vifaa hivi ili kuimarisha usafi kwa walimu na wanafunzi katika shule zote za serikali Kata ya Makongo. UWT tunatambua wajibu wetu katika suala zima la malezi kwa watoto, hivyo vifaa hivi vitawasaidia kudumisha usafi shuleni,”anasema Abriat.
Ameeleza kukabidhi vifaa hivyo siyo mwisho bali UWT Kata ya Makongo itaendelea kusimamia kikamilifu malezi na kudumisha usafi shuleni.
“Tumekabidhi mifagio, sabuni za chooni, makopo na kufanya usafi katika vyoo vya walimu na wanafunzi,”ameeleza.
Mwenyekiti huyo amedai UWT Kata ya Makongo, waliona ni vema kusherehekea kwa njia tofauti Wiki ya UWT kwa kutoa vifaa vya usafi badala ya kushiriki kufanya usafi pekee.
Katibu wa UWT wa Kata ya Makongo, Deodata Komba, ametaja shule zilizonufaika kuwa ni Shule za Msingi Changanyikeni, Makongo na Londa ambapo kwa upande wa Sekondari ni Makongo Juu.
Wakipokea vifaa hivyo, walimu, wanafunzi na wajumbe wa kamati za shule hizo wameishukuru UWT Kata yaMakongo na kudai vifaa vimefika wakati muafaka ambapo jamii inapambana na maambukizi ya virusi vya Uviko-19 .
“Katika mazingira kama haya yenye tishio la Uviko-19 usafi ni jambo la msingi mno kwa walimu na wanafunzi.
Vifaa hivi vitasaidia kudumisha usafi shuleni hivyo kuwakinga walimu na wanafunzi dhidi ya maambukizi yakiwemo ya Uviko-19,”ameeleza Mjumbe wa Kamati ya Shule ya Msingi Changanyikeni, Elitia Sirro.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Makongo, Joyce Kimaro amedai , UWT Makongo, imeonyesha ukomavu hususan wakati huu ambapo taifa linaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kitendo cha kukabidhi vifaa hivyo kimewatia moyo.
Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya UWT kinafanyika kesho ambapo katika Mkoa wa Dar es Salaam, maadhimisho hayo yanafanyika Wilayani Ubungo.