Dkt. Joseph Mdachi alitoa elimu na kuhamasisha wananchi juu ya chanjo ya Uviko-19 katika Mtaa wa Chinyika, Kata ya Mkonze
Mwenyekiti wa Mtaa wa Chinyika, Kombo Ally Kombo (katikati) akiongoza kikao cha Mtaa. Kulia ni Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Chinyika, Olympia Matoly
****************************
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Serikali imeamua kutoa chanjo ya Uviko-19 kwa wananchi wake ili kuwahakikishia maisha bora kwa kuzuia vifo vitokanavyo ya ugonjwa huo.
Kauli hiyo ilitolewa na mtaalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Joseph Mdachi alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Mtaa wa Chinyika, Kata ya Mkonze jijini Dodoma katika siku ya pili ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo ya Uviko-19.
Dkt. Mdachi alisema kuwa chanjo ya Uviko-19 ni kama chanjo nyingine zinazotolewa nchini. “Chanjo hii inatolewa kwenye vituo vilevile na watoa huduma ni walewale na inahifadhiwa kama chanjo nyingine. Serikali imeamua wananchi wake wapate chanjo hii ili kupunguza na kuzuia kabisa maambukizi na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Uviko-19 nchini” alisema Dkt. Mdachi.
Akiongelea usalama wa chanjo hiyo, alisema kuwa chanjo hiyo ni salama. Baada ya serikali kufanya utafiti na kujiridhisha kuwa chanjo hiyo ni salama ndiyo iliruhusu iingie nchini na watanzania waweze kuchanja. “Dodoma hii watu takribani 13,000 wamechanja chanjo hii. Watu hawa tunawafahamu kwa majina. Tunapochanja tunafuatilia kama kuna aliyepata shida au madhara kutokana na chanjo hiyo. Nataka niwahakikishie hakuna mtu aliyepata madhara baada ya kuchanja kwa Halmashauri yetu ya Jiji la Dodoma” alisema Dkt. Mdachi.
Mtaalam huyo alisema kuwa yupo kwa ajili ya kutoa elimu na kufafanua maeneo ambayo wananchi watakuwa wanahitaji ufafanuzi juu ya chanjo.
“Mimi na wataalam wenzangu tunawashauri mchanje kwa sababu ugonjwa wa Uviko-19 unakuja kama wimbi. Wimbi likiibuka linaua watu wengi na kuacha majanga katika familia na taifa kwa ujumla. Ndugu zangu mkiona hadi Rais wa nchi anakwambia chanja, wewe chanja. Usisubiri wimbi lingine, wimbi linapotokea hewa ya “Oxygen” ni shida kuipata jamani” alisema Dkt. Mdachi kwa sauti ya upole na kuonesha kujali maisha ya watu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Chinyika, Kombo Ally Kombo alisema kuwa mtaa wake una bahati sana. “Serikali iliweka kutuo cha kupokea na kutibu wagonjwa wa Uviko-19 hapa. Na leo bahati nzuri tumeletewa chanjo hapa Mkonze. Hii ni fursa kwetu kwa sababu hakuna foleni wakati wa kuchanja. Tutumie fursa hii kabla wengine wa mbali hawajaja kunufaika na fursa hii” alisema Kombo kwa kujiamini.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea na utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo ya Uviko-19 kwa kutembelea taasisi mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha na kutoa huduma ya chanjo kwa watakaohamasika ikiwa katika siku yake ya pili.