**************************************
MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akiwa Wilayani Mpwapwa katika Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) amepokea wanachama wapya wa CCM 32 na wanachama wapya 130 wa UWT ambapo pia ameahidi kutoa mifuko 50 ya Saruji na matofali 500 kwa kwa kila Wilaya ya Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba za Makatibu wa UWT Wilaya.
Ditopile amepokea wanachama hao na kutoa mchango wake huo kwa UWT ambapo alialikwa kuwa mgeni rasmi kwenye Wiki ya UWT ambayo kiwilaya ilifanyika katika Kata ya Mazae ambapo amesisitiza Wanawake kutumia asilimia 10 ya fedha zinazotolewa na Halmashauri kama mikopo kwa Vijana, Wanawake na Walemavu ili kufanya miradi itakayowaingizia kipato.
Amesema ni wakati wa Wanawake kumuunga kwa nguvu Rais Samia Suluhu Hassan ili kumtia moyo katika utekelezaji wa majukumu yake ambapo ameonesha pamoja na kuwatumikia watanzania pia ameamsha ari kwa mabinti nchini kujikita katika uongozi.
“Sisi kama Wanawake tunajivunia kupata Rais wa kwanza mwanamke kwenye Nchi yetu, ni lazima tumuunge mkono tumtie nguvu ili azma yake njema aliyonayo. Tumeona ndani ya muda mfupi ametoa Trilioni 1.5 kwa Wabunge wote Nchi nzima kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Barabara, pia ameahidi kufikia Januari mwakani atakua amekamilisha ujenzi wa Madarasa 15,000 Nchi nzima.
“Niwasihi Ndugu zangu suala la UVIKO-19 msilichukulie poa, ugonjwa huu upo na unaua, Niwaombe kuchukua tahadhari. Rais Samia ameleta chanjo twendeni tukachome, msiwasikilize wapotoshaji wanaosema chanjo ni mbaya, Hii chanjo imethibitishwa na wataalamu wetu na Rais akaruhusu wananchi tutumie, Lakini pia niwasihi zoezi la Sensa likianze tujitokeze pia kuhesabiwa,”Amesema Ditopile.
Mbunge huyo pia ameahidi wananchi hao kupokea changamoto ya ujenzi wa Zahanati yao ya Kata ya Mazae.
” Niwaahidi nalichukua na nitawasiliana na Waziri Ummy ili kama Serikali waangalie namna gani ya kumaliza ujenzi wa Zahanati hii ili akina Mama wasitembee umbali mrefu kwenda kujifungua, Lakini sambamba na hilo na mimi kama Mbunge nitaweka nguvu yangu hapa,” Amesema Ditopile.