Timu ya Yanga imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kupata ushindi wa pili mfululizo kwa kuichapa bao 1-0 Geita Gold Mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara uliochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Bao la Yanga na la ushindi limefungwa na winga wao hatari Jesus Moloko dakika 16 baada ya kuunganisha krosi ya Mshambuliaji Yacoub Songne .
Kwa Matokeo hayo Yanga imefikisha Pointi 6 na kushika nafasi ya pili na nafasi ya kwanza inashikwa na Polisi Tanzania wenye Pointi 6 sawa na Yanga ila wana mabao mengi ya kufunga.
Mechi nyingine za Leo Ligi Kuu Coastal Union wakiwa uwanja wao wa nyumbani wamepata sare ya pili baada ya kushindwa kupata ushindi dhidi ya KMC mchezo uliomalizika bila kufungana uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Matajiri wa Chamazi timu ya Azam imeshindwa kutamba ugenini baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Polisi Tanzania mabao ya wenyeji yakifungwa na Kassim Shaban dakika ya 23 na Adam Adam dakika ya 40 huku la Azam likifungwa na Idd Nadp dakika ya 29 mchezo uliopigwa katika uwanja wa Ushirika Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Kwa ushindi huo Polisi Tanzania wamefikisha Pointi 6 na kuongoza Msimamo wa Ligi baada ya kushinda mechi mbili wakiwa na mabao ya kufunga manne na kufungwa moja.