…………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WANAWAKE wa kikundi cha Magonga B wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, Salome Nelson Mnyawi, wametoa msaada wa chakula, kwa shule mbili za msingi za Kata hiyo.
Wanawake hao wa Magonga B wametoa msaada huo wa chakula kwa shule za msingi Songambele na Tanzanite mbele ya Afisa mtendaji wa kata ya Mirerani, Abraham Malamia, Afisa elimu kata Dinnah Mbise na wenyeviti wa vitongoji Boaz Amboya, Jotham Lolo na Christopher Chengula.
Msaada huo wa chakula umetolewa magunia manne ya mahindi, mawili ya maharage na sukari kilo 50 ambapo shule ya msingi Tanzanite imepatiwa magunia mawili ya mahindi, moja la maharage na sukari kilo 25, shule ya Songambele magunia mawili ya mahindi, moja la maharage na sukari kilo 25.
Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi, akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo amesema kupitia kikundi chao cha wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite cha wanawake wa Magonga B waliona warudishe kidogo walichokipata kwa jamii.
Amesema waliamua kama kikundi wanunue vyakula hivyo na kutoa msaada kwa wanafunzi wa shule hizo mbili za Tanzanite na Songambele ili kutoa hamasa ya chakula shuleni wakati wa masomo.
“Chakula kikiwa shuleni hata utoro utapungua kwani wanafunzi watakuwa na uhakika wa kula chakula na baadhi ya wenye changamoto ya kutokula nyumbani watapata shuleni na kusoma kwa bidii,” amesema Salome.
Makamu Mwenyekiti wa mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, Christopher Chengula amemshukuru Diwani wa kata hiyo Salome Mnyawi na kikundi cha wanawake cha Magonga B kwa kufanikisha msaada huo wa chakula kwa wanafunzi wa shule hizo.
“Nikiwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Tunduru, kwa niaba ya wenyeviti wenzangu, tunakushukuru mno mheshimiwa Diwani Salome na wakina mama wenzako kwa msaada huu,” amesema Chengula.
Afisa mtendaji wa kata ya Mirerani, Abraham Malamia amesema upendo wa Diwani wa kata hiyo Salome Mnyawi na wakina mama wa kikundi cha Magonga B kwa wanafunzi wa shule hizo zimeonekana dhahiri.
“Wanavikundi, taasisi, mtu mmoja mmoja wanapaswa kuiga mambo mazuri kama haya ya kuwajali wanafunzi wetu kwa kununua chakula ambacho kitaliwa shuleni hapo na wanafunzi hao,” amesema.
Afisa elimu wa kata ya Mirerani, Dinnah Mbise amewapongeza wanawake hao wa kikundi cha Magonja B kwa kukabidhi msaada wa chakula kwa wanafunzi wa shule hizo.
“Kweli wanawake ni jeshi kubwa kinamama wa Magonga B na Diwani wetu Salome tunawapongeza kwa msaada huo ambao kwa namna moja au nyingine utaongeza jitihada za wanafunzi kusoma kwa bidii,” amesema Mbise.