Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisalimiana na wakandarasi na wasimamizi wa mradi wa upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha (km 19.2) kuwa njia nane, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Elisony Mweladzi, wakati akikagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha (km 19.2) kuwa njia nane, jijini Dar es Salaam.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Elisony Mweladzi (kulia), akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (kushoto), wakati akikagua mradi huo ambao ujenzi wake umefikia asilmia 94, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa moja ya Daraja la juu la Kibamba lililokamilika kujengwa kama sehemu ya mradi wa upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha (km 19.2), jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa barabara ya Morogoro (Kimara – Kibaha) kilometa 19.2 baada ya kupanuliwa na kuwa njia nane ambapo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 94.
PICHA NA WUU
………………………………………………………………………..
Serikali imewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia misingi na maadili ya taaluma yao pindi wanapotekeleza majukumu yao pasipo kuleta taharuki kwa jamii na Taifa.
Aidha, waandishi hao wameaswa kupata taarifa sahihi hasa za miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Serikali kupitia vyanzo sahihi kabla ya kusambaza kwa jamii.
Amesema hayo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, wakati akikagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa barabara ya Morogoro (Kimara – Kibaha) km 19.2 kuwa njia nane ambao ujenzi wake umefikia asilimia 94 na kubakiza kazi ndogondogo ambazo zinatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Disemba, 2021.
“Ili kupunguza taharuki kwenye jamii kuhusu miradi ya maendeleo nchini, waandishi wa habari wazingatie miongozo inayoongoza taaluma zao na kufikisha taarifa hizo kwa usahihi na kupata taarifa kutoka vyanzo husika”, amesisitiza NaibuWaziri Waitara.
Ameongeza kuwa mkandarasi haidai Serikali na tayari amekwishalipwa kiasi cha shilingi Bilioni 149.8 kati ya Shilingi Bilioni 161.4 ambazo ni sawa na asilimia 92.78.
Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Elisony Mweladzi, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa kumekuwa na ongezeko la kazi katika mradi huo ambao ni ujenzi wa madaraja mawili ya juu eneo la Mbezi mwisho ili kupunguza msongamano katika kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli.
Kazi nyingine ni ujenzi wa barabara ya maingilio katika kituo cha mabasi cha Magufuli, ujenzi wa barabara za maingilio kwenda ofisi za Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, umaliziaji wa barabara ya huduma (service road) eneo la kibaha, taa za kuongoza magari na ujenzi wa vituo vya mabasi na daladala eneo la Kibamba ili kutoa huduma kwa abiria wanaokwenda hospitali ya Mloganzila.
Kwa upande wake, Meneja wa mradi kutoka kampuni ya Estim, Mhandisi Freddy Nyenga, amesema kazi zinaendelea vizuri na mpaka sasa hawaidai Serikali na kazi zilizobakia ni zile za ongezeko la kazi.
Mradi wa upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha (km 19.2) umehusisha ujenzi wa njia sita (tatu kila upande) zenye urefu wa kilometa 19.2, ujenzi wa njia za maingilio, njia za watembea kwa miguu, makutano yenye taa na ’roundabouts’, miundombinu ya maji ya mvua, daraja la wavuka kwa miguu eneo la Mbezi Mwisho, Daraja la juu Kibamba CCM na ujenzi wa madaraja sita (mawili eneo la kibamba, mawili eneo la Kiluvya na mawili eneo la Mpiji).
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi