…………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Babati
MKUU wa Jimbo la Babati wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mchungaji Robert Mallya ameipongeza shule ya awali na msingi Tarangire ya mchepuo wa kiingereza kwa kuendelea kuwalea wanafunzi wao kwenye maadili mazuri na ya kumpendeza Mungu.
Mchungaji Mallya ameyasema hayo wakati akizindua vyumba vipya vya madarasa kwenye mahafali ya tatu ya wahitimu wa darasa la saba wa shule hiyo ya awali na msingi Tarangire.
Mchungaji Mallya amesema licha ya shule hiyo kuendelea kufanya vyema kitaaluma, imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na viongozi wa madhehebu mbalimbali katika kuhakikisha wanafunzi wao wanajengwa kiroho.
“Mahafali hayo ni mwanzo tuu wa msingi kwani Mungu akiwa upande wako hakuna atakayeweza kuwabadilisha watoto hawa ambao wamekuwa na nidhamu ya kipekee na walimu wa shule hii ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwaongoza watoto hawa,” amesema.
Amewataka wazazi na walezi wawe makini na watoto hao kwani hivi sasa wanaenda mitaani hivyo waendeleze maadili mazuri waliyoyapata shuleni hapo ambapo amewaambia mistari ya Biblia inasema Mungu akiwa yuko upande wao ni nani aliye juu yao.
Ofisa Tawala wa Wilaya ya Babati, Salum Issa, akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi wa mahafali hayo, Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange amewapongea wanafunzi hao kwa kuvumilia hadi kuhitimu darasa la saba kwani wakiendelea kuwa wavumilivu watatimiza malengo yao.
Issa amesema utengano uliokuwa zamani hasa katika kubagua nyanja ya elimu kwa mtoto wa kike na kiume umeisha na sasa mambo ya mila na desturi yamebadilika kutokana na ongezeko la teknolojia hivyo kusababisha watoto wa kike kusoma kwa bidii na kuwa viongozi bora.
Amesema suala la miundombinu ya barabara kuna mradi unaendelea wa ujenzi wa barabara katika wilaya hiyo ambapo barabara za Mamire, Endanachan na Riroda zipo kwenye mpango mkakati wa ujenzi huo.
Mkurugenzi wa Shule hiyo, Ronald Paul amesema shule hiyo inafundisha elimu bora ikiwemo maadili mema hivyo wazazi, walezi na wote wenye watoto wanapaswa kuwapeleka shuleni hapo wakasome.
Paul amesema shule ya awali na msingi Tarangire, ina walimu bora wenye ujuzi wa kufundisha taaluma, ina mazingira bora na hali nzuri ya hewa iliyopo chini ya mlima Kwaraa.
Amesema shule hiyo ipo Mjini Babati, kwenye mtaa wa Wang’waray, mbele kidogo ya chuo cha ufundi stadi (Veta) Manyara, hivyo wazazi na walezi wawapeleke watoto wao hapo kwani wana wanafunzi wa bweni na wa kutwa.
Wahitimu wa darasa la saba wa shule hiyo wamewashukuru walimu wao kwa kuwapa malezi bora na kuwafundisha masomo ya ujasiriamali ambayo yatawasaidia kwa maisha yao ya baadaye.
Hata hivyo wameahidi kufaulu kwa kupata daraja la kwanza kwani kwenye taaluma wamekuwa wakifanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya kata amabayo wamekuwa wakishindanishwa na shule nyingine za mjini Babati.