Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Mkoani Mtwara Abdallah Chikota akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mnyahi Kata ya Milango Minne Katika Halmashuri ya Nanyamba Mji alipofika kusikiliza kero za wananchi hao, kueleza mipango ya Serikali katika kutekeleza ahadi ambazo chama Tawala cha CCM kiliahidi wakati wa kampeni
Wakazi wa Kijiji cha Mnyahi wakieleza kero zao Kwa Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Mkoani Mtwara Abdallah Chikota aliyefika kijijini hapo kusikiliza kero za wananchi hao na kueleza mipango ya Serikali katika kutekeleza mipango ya maendeleo iloyoahidiwa na CCM wakati wa kampeni.
…………………………………………………………….
Na Mwaandishi Wetu Mtwara
MBUNGE wa Jimbo la Nanyamba mkoani Mtwara Abdallah Chikota amesema ahadi zote ambazo Chama Cha Mapinduzi(CCM) kiliahidi kwa wananchi wa jimbo hilo wakati wa kampeni zitatekelezwa na kukamilika kama ilivyopangwa.
Chikota ametoa maelezo hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kata ya Milango Minne kwenye Halmashauri ya Nanyamba Mji Mkoani humu.
“Ahadi zote tulizowaahidi wakati wa kampeni tutazitekeleza, zile alizoahidi mama Samia akiwa mgombea mwenza zinatekelezwa kwa sasa na CCM itahakikisha zinakamilika kama ilivyopangwa,” amesema,
Chikota amesema Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwa mgombea mwenza alitoa ahadi za kitafa ikiwa ni pamoja na ahadi ya ujenzi wa barabara kutoka Mnivata Halmashauri ya Nanyamba mpaka wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara.
Amesema Benki ya Maendeleo ya Africa tayari imeshaidhinisha fedha kwa ajili ya kujenga kilomita 110 kutoka Mnivata mpaka Masasi huku akifafanua ujenzi huo utahusisha wakandarasi watatu ili kuharakisha kazi.
Kwa hatua nyingine Chikota amesema Rais ametoa Sh.bilioni moja kwa kila jimbo nchini ili kukarabati, kujenga na kuboresha barabarani za vijijini kwenye majimbo hayo.
Chikota ameeleza fedha hizo zitatumika kukarabati na kuimarisha barabarazote ambazo zilikuwa hazifanyiwa ukarabati.
“Mama Samia ametoa fedha Sh.bilioni moja kwa kila jimbo kuimarisha barabara za vijijini na kwa jimbo letu sisi hizo fedha zitasaidia kuhakikisha barabara zote ambazo zilikuwa hazichongwi kila mwaka mwaka huu zitachongwa,” amesema.
Amesema Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini TARURA jimboni humu walikuwa na bajeti ya milioni saba na kwamba sasa bilioni moja aliyotoa Raisi Samia kwa jimbo hilo zitaongeza ukubwa wa kazi ambayo TARURA watafanya katika kukajenga barabara hizo za Nanyamba.
Pia aliwaambia wananchi wa jimbo lake kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ahadi zingine ikiwa ni pamoja ya kuhakikisha kila kijiji kinapata kama CCM ilivyoahidi.
Amesema jimbo hilo lina vijiji 44 ambavyo bado havijaunganishwa na umeme huku akisema kuwa wakandarasi wapo kwenye vijiji hivyo wakiendelea kufanya taratibu za kuunganisha umeme kwenye vijiji hivyo.
“Mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili, tulizindua hapa kwa jirani zetu namtumbuka, na wakandarasi wako kwetu kwa wamekuja kufanya ‘survey’ hapa, tulikuwa na vijiji themani na saba vyote vilikuwa havina umeme wakati huo, sasa hivi tumebakia na vijiji arobaini nan ne tu,” amesema.
Katika hatua nyingine Chikota amewaambia wananchi wa jimbo hilo kuwa Raisi ametoa pesa kwa ajili ya kugharamia salpha na madawa mengine ya kuua wadudu kwenye mikorosho huku akisistiza kuwa dawa hizo zinatolewa bure kwa wakulima na kwamba hakuna atakayekatwa pesa hizo.
“Wewe mkulima wakati wa kuuza korosho yako hutakatwa hata shilingi na ukikatwa nipigie sim, mama Samia alitoa pesa bure kwa mapenzi yake kwa wakulima wa wakorosho,”amesema.