Kushoto ni Dkt Agnes Gidna akimpatia maelezo Mkuu wa Wilaya wa Lindi Mhe Shahibu Ndemanga (wapili kushoto) kuhusu mfupa wa Dinosaria uliogundulika Tendaguru Lindi. Wapili kulia ni Katibu Tawala Wilaya ya Lindi Mhe Thomas Safari na kulia ni Kamanda wa Polisi Wilaya ya Lindi
Dkt Amandusi Kweka mwenye nyundo kiunoni akimpatia maelezo Mkuu wa Wilaya wa Lindi Mhe Shahibu Ndemanga (mwenye kofia) kuhusu mifupa ya Dinosaria iliogundulika Tendaguru Lindi alieshika kiuno ni Msimamizi Mkuu wa Utafiti wa Mashirikiano ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam Dkt Frank Masele
Sehemu ya mfupa wa mguu wa Dinosaria alieishi miaka milioni 150 iliyopita ambao umegundulika huko Tendaguru Lindi.
Wanahabari kutoka nchini Ujerumani na wa hapa nchini wakifuatilia maelezo ya Mkuu wa Wialaya ya Lindi Mhe Shaibu Ndemanga alietembelea eneo la Tendaguru kulipo patikana masalia mapya ya Dinosaria walioishi miaka milioni 150 iliyopita huko Mkiani Lindi
………………………………………………………….
Na Sixmund J. Begashe
Watafiti kutoka Makumbusho ya Taifa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wa nchini Ujerumani, wamegundua masalia mapya ya Mijusi mikubwa aina ya Dinosaria walioishi miaka milioni 150 liyopita huko Lindi maeneo ya Tendaguru.
Akielezea matokeo ya utafiti huo Mhifadhi na Mtafiti Mwandamizi wa Akiolojia Makumbusho ya Taifa Dkt Agnes Gidna, amesema amesema japokuwa wamechukuwa muda mfupi katika kufanya utafiti hadi sasa wamepata mifupa ya sehemu mbalimbali za Mijusi hiyo ikiwepo ya Miguu, mbavu na mgongo kwa ujumla inauzito wa takribani tani mbili.
“Matokeo haya ni muhimu sana na yanatupa faraja kuwa Tanzania itakuwa kinara cha utalii wa Dinosaria pamoja na kuwavutia watafiti wengine wengi, masalia haya tulioyagundua yanaonesha ni Mjusi Mkubwa sana yawezekana akawa mara tatu ya ukubwa wa tembo, anafanana na yule aliehifadhiwa nchini Ujerumani” Aliongeza Dkt Gidna.
Msimamizi Mkuu wa Utafiti wa Mashirikiano ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam Dkt Frank Masele ameelaza ni tafiti chache zilizo fanyika maeneo ya Lindi na Mtwara zinazo husu Akiolojia licha ya maeneo hayo kuwa na utajiri Mkubwa katika nyanja hiyo, hivyo kwa utafiti unaoendela sasa utakuwa kichocheo cha watafiti wengine.
“Zamani tafiti zilifanywa na taasisi za nje lakini sasa taasisi za ndani zinafanya tafiti hizi hasa kwa kushirikiana kama hivi sasa tunashirikiana na Makumbusho ya Taifa na wenzetu kutoka Ujerumani yote ni kupata matokeo chanya katika kazi hii kama walivyo fanikiwa wale watafiti wa huko nyuma”. Dkt Masele
Naye Mtafiti kutoka Makumbusho ya Naturkunde Berlin nchini Ujerumani, Dkt Daniela Schwarz, ameeleza faraja ya mashirikiano yao na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wa Mkumbusho ya Taifa kwani yanaimarisha mshikamano zaidi katika familia ya wana Akiolojia Duniani hasa wa nchi hizi mbili.
Akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Lindi katika eneo hilo la Tendaguru, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Shaibu Ndemanga licha ya kuwapongeza watafiti hao kwa kazi nzuri wanayoifanya, amesema Serikali imeshachukuwa hatua za awali za kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama na haliharibiwi na mifugo pamoja na watu wa maeneo hayo.
Mhe. Ndemanga aliongeza kuwa Serikali pia inaendela kuhakikisha miundombinu hususan barabara zinakuwa rafiki kwa watafiti na watalii watakaoenda eneo hilo pamoja na kutoa wito kwa watu mbalimbali kwenda kutalii kwenye eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa historia ya Dinosaria.