*************************************
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote duniani katika kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Matumizi Sahihi ya Kidigitali kwa Ustawi wa Rika zote.” Kauli mbiu hii inalenga kuhakikisha kuwa matumizi ya kidigitali yanachangia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, wakiwemo wazee na kuchochea ubunifu kwa shughuli zinazolenga kuimarisha usitawi wa wazee na wananchi wote. Katika maadhimisho haya wadau katika maeneo mbalimbali nchini hupata fursa ya kukutana na kubadilishana mawazo kuhusiana na mustakabali wa haki na ustawi wa wazee kwa ujumla.
Katika matumizi ya teknolojia Serikali imechukua hatua kadhaa, ikiwemo kukamilisha mkongo wa taifa wa mawasiliano ambapo mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar imeunganishwa na kuwezesha uwepo wa kampuni mbalimbali za mawasiliano (Telecom Operators and Internet Service Providers) ambazo zimeunganishwa kwenye mkongo huo. Hatua hizi zimetoa fursa kwa wananchi wengi, wakiwemo wazee kutumia huduma za kimtandao kutatua changamoto zinazowakabili na hivyo kujiletea maendeleo.
Hata hivyo, jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa katika kuboresha matumizi ya teknolojia kwa wazee kwa kuwa idadi ya wazee imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Tanzania ilikuwa na jumla ya wazee 2,507,508 ambapo wanawake walikuwa 1,307,358 na wanaume 1,200,210, na hadi mwaka 2021 idadi hiyo imeongezeka. Ongezeko la wazee huashiria uhitaji wa ongezeko la huduma mbalimbali kwa wazee ikiwemo huduma za kidigitali.
Tume inaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua zilizochukuliwa katika kuboresha maisha ya wazee hapa nchini ili kuhakikisha wanapata huduma jumuishi na stahiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wazee kuwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia Tume inaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutunga Sheria ya Masuala ya Wazee Na. 2 ya mwaka 2000; kuweka utaratibu wa kuwapatia pensheni jamii na vitambulisho vya kupatiwa huduma mbalimbali wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70.
Aidha, Tume inazipongeza Serikali zote mbili kwa kuendelea kutoa huduma ya matunzo, ulinzi na usalama kwa wazee wote. Huduma hizi zimesaidia kupunguza vifo na mauaji kwa wazee hapa nchini. Hata hivyo, jitihada hizo zitaimarika zaidi endapo kutakuwa na matumizi mazuri ya teknolojia hasa baada ya Serikali zote mbili kuwekeza zaidi kwenye Sekta hii.
Pamoja na jitihada hizo, bado wazee wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kutokuwepo kwa Sheria mahsusi ya wazee, kuchelewa kwa malipo ya mafao kwa wastaafu na upatikanaji wa madawa na vifaa tiba kwa wazee. Hivyo, Tume inatoa rai kwa:
- Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukamilisha mchakato wa mapitio ya Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 kwa kushirikiana na wadau, ili Sheria inayosimamia masuala yote ya wazee iweze kuandaliwa.
- Serikali kuongeza jitihada kutatua changamoto za upatikanaji wa dawa katika hospitali na zahanati ili wazee wafaidi huduma hizo kama ilivyokusudiwa.
- Serikali kuhakikisha mafao ya wastaafu yanalipwa kwa wakati ili kuwaondolea wazee usumbufu wa kufuatilia.
- Wananchi wa rika zote kuwa na matumizi mazuri ya teknolojia, kwani matumizi mabaya hupelekea kuvuruga ustawi wa wananchi wakiwemo wazee.
- Wadau wote wa masuala ya kidigitali kutii Sheria inayosimamia sekta ya mawasiliano nchini ili kuwepo na matumizi sahihi ya teknolojia na kuhakikisha kuwa haki za wananchi wa rika zote wakiwemo wazee hazivunjwi bali zinadumishwa na kulindwa.
- Serikali na wananchi wote kwa ujumla kulinda na kutetea haki za wazee, ikiwemo kuthamini mchango, uzoefu na ushiriki wao kwa maendeleo ya taifa.
“Tanzania yenye matumizi sahihi ya kidigitali kwa ustawi wa rika zote inawezekana endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake.”