Na.Alex Sonna,Dodoma
Hivi ndivyo! unaweza kusema Mabingwa watetezi,Simba SC wamefufuka ugenini baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Dodoma Jiji FC mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliopigwa katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Timu zote zilianza kwa kushambuliana kwa kasi huku Dodoma wakicheza rafu nyingi zilizosababisha mshambuliaji wao ,Anuary Jabir kutolewa kwa kadi nyekundu mnamo dakika ya 41 baada ya kumpika kiwiko beki wa Simba, Kennedy Juma ambaye alishindwa kuendelea na Mchezo.
Mpaka kipindi cha kwanza wanaenda mapumziko hakuna timu ambayo ilikuwa imeshapata bao na kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Simba wakifanya mabadiliko kwa kuongeza idadi ya washambuliaji na kuwa watatu.
Mabadiliko hayo yaliweza kuisaidia Simba mnamo dakika ya 70 Mshambuliaji hatari
, Meddie Kagere aliwanyanyua mashabiki wake akimalizia pasi ya kichwa ya
Chris Mugalu
Kwa ushindi huo Simba imefikisha pointi nne na kuongoza Ligi hiyo baada ya mechi mbili za mwanzo kufuatia sare ya bila kufunga na wenyeji,Biashara United mchezo wa kwanza mjini Musoma mkoani Mara huku Dodoma wakibaki na Pointi zao tatu walizozipata kwa Ruvu Shooting.
Mchezo Mwingine wa Ligi Kuu Wazee wa kupapasa Ruvu Shooting wamepata ushindi ugenini kwa kuwachapa wenyeji Biashara United bao 1-0 lililofungwa na winga , Rashid Juma dakika ya 47 Uwanja wa Karume mjini Musoma.
Ligi Kuu ya Tanzania bara inatarajia kuendelea kesho Yanga baada ya kupata ushindi ugenini dhidi ya Kagera Sugar,watakuwa katika uwanja wa Benjamini Mkapa kucheza na wageni wa Ligi hiyo Timu ya Geita Gold kutoka Mkoani Geita majira ya saa moja usiku.
Matajiri wa Chamazi baada ya kuanza kwa sare ugenini kesho watatupa karata yao ya pili uwanja wa Karatu kucheza na wenyeji Polisi Tanzania majira ya saa kumi jioni.
Mechi ya mapema itachezwa uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga wenyeji Coastal Union watawakaribisha vijana wa Kinondoni KMC majira ya saa nane Mchana.