Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, akielezea maagizo sita aliyotoa ili kuboreshwa soko la madini ya Tanzanite, Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, kushoto ni msaidizi wake Mussa Mgogosi.
*************************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Mkoa wa Manyara, RC Charles Makongoro Nyerere, ametoa maagizo sita kwa sekretarieti ya Mkoa huo na viongozi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani ili kuboresha soko la madini ya Tanzanite.
RC Makongoro amesema miongoni mwa maagizo hayo ni upatikanaji wa hatimiliki wa ekari 250 za eneo lililotengwa la ujenzi wa soko hilo.
Amesema hati hizo za ekari 250 zitakabidhiwa kwa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro na ameagiza baada ya wiki tatu hati miliki hizo ziwe zimekamilika na wahusika kukabidhiwa.
“Baada ya hati hizo kupatikana shughuli ya ujenzi wa magorofa mawili ya Tanzanite city zitaanza mara moja ili ofisi mpya za masoko ya madini zijengwe,” amesema Makongoro.
Amesema pia ameagiza apatiwe taarifa kamili ya gharama za ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa ya Tanzanite city, ambayo yatakuwa soko la wadau wa madini ya Tanzanite.
“Mara baada ya kupatikana kwa hati hizo Wizara ya Fedha na Mipango itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo mawili makubwa ya ghorofa,” amesema Makongoro.
Amesema pia ameagiza kuundwa kwa kamati tatu ikiwemo kamati ya ujenzi, kamati ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi na kamati ya mapokezi na amewapa ridhaa ya kufanya kazi.
Amesema pia ameagiza usalama uboreshwe kwani hivi sasa madini ya Tanzanite yanasafirishwa duniani kutoka Mirerani mara baada ya ofisa madini mkazi Fabian Mshai kutoa kibali.
Amesema hivi sasa wadau wa madini wanaendelea na biashara yao ya madini ya Tanzanite kwenye soko lililopo benki ya NMB na soko la mfanyabiashara Paul Mollel.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Mashaka Jororo amesema jitihada za serikali zinaonekana katika kufanikisha ukamilishaji wa soko la madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani.