Matukio katika ziara ya mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akiwa kata ya Mbwawa (picha zote na Mwamvua Mwinyi)
******************************
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini,Silvestry Koka , ametoa rai kwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira ( DAWASA), kuangalia mfumo rahisi wa kuunganishia wananchi huduma ya maji safi katika kata ya Mbwawa,ili kupunguza gharama kubwa ya usambazaji maji.
Ameeleza hatua hii itawezesha malengo ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kumtua ndoo mama kichwani kufanikisha pasipo kuweka gharama kubwa zinazowabana watumiaji ambao wengi wao wana uwezo duni .
Koka alitoa rai hiyo katika ziara yake kata ya Mbwawa, ambapo alipokea malalamiko ya mradi wa maji Mlandizi-Mbwawa unajengwa kwa bilioni 1.1 ambao bado hautoi maji ya uhakika licha ya kuwa kwenye hatua ya usambazaji kwa wateja.
Kufuatia kero hiyo ,mbunge huyo ameunda kamati itakayoanza kazi mara moja kufuatilia changamoto hizo kwa meneja DAWASA na ikishindikana kufika kwa mkurugenzi mtendaji ili kupata ufumbuzi .
“Dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini yake Samia Suluhu Hassan ni kuona miradi ya maji inaleta matokeo na tija kwa wananchi ,Itakuwa ni mchezo kama miradi inayogharimu fedha nyingi kukamilika pasipo wananchi kunufaika nayo “alifafanua Koka.
Aidha Koka aliwaagiza watendaji wa kata na maeneo ya pembezoni, wasiwe chanzo Cha migogoro ya wakulima na wafugaji na kuwataka wachukue hatua kuondoa kero hiyo kandamizi kwa wakulima.
Pamoja na hayo ,alisema anaendelea kupigania barabara kwa kiwango cha lami Mlandizi -Makofia ili fedha itoke na kuanza ujenzi ,na kuongeza ni barabara ambayo ipo katika utekelezaji wa ilani hivyo wananchi wavute subira.
Koka alieleza ,kwasasa lengo lake ni kuona kata za pembezoni ikiwemo Mbwawa inasogezewa huduma za kijamii kwa kasi kama shule za sekondari,vyuo,vituo vya polisi ,maji na umeme kama ilivyo kata zilizopo mjini .
Katika hatua nyingine Koka aliwaasa ,wananchi kulinda mali na miundombinu ya miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji na kuacha udokozi kwani kunakwamisha utekelezaji wa miradi .
Akijibu kuhusiana na changamoto za mradi wa maji, mwakilishi kutoka DAWASA ,Yohana alisema suala hilo lipo ndani ya uwezo wa meneja DAWASA.
Alisema pia tatizo la kupasuka kwa mabomba chakavu yaliyo katika mtandao wa zamani linashughulikiwa ili kupata maji ya uhakika .
“Mbwawa ilikuwa haina maji ,tulianza na wateja 159 hadi Mbwawa Miswe kuwaingiza kwenye mtandao wa zamani walikuwa wanapata maji Bagamoyo,Ila chanzo Cha Bagamoyo hakikidhi Cha Mlandizi ndicho cha uhakika”alieleza Yohana.
Awali diwani wa kata ya Mbwawa Judith Mluge alisema, wanakabiliwa na changamoto ya mabomba kupasuka mara kwa mara hali inayosababisha kukosa maji ,ukosefu wa shule ya sekondari.
Wakazi wa Mbwawa Asha Matambo,Mzee Shomali walibainisha ,wanatakiwa kulipia gharama za kuunganishiwa maji sh.200,000- 800,000 kwa umbali wa mita tano kiasi ambacho ni kikubwa.