Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassana Abbasi akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo pichani) Kuhusu Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Viziwi Afrika itakayofanyika kesho Oktoba 1, 2021 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Tanzaania, kuanzia saa 1:00 jioni.
*********************************
Na Eleuteri Mangi, WSUM
Tanzania imejipanga vyema na ipo tayari kwa Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Watu Wenye Usikivu Hafifu (Viziwi) Afrika yatakayofanyika Oktoba 01, 2021 katika Ukumbi Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utanaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi wakati wa mkutano na waandishi wa habari Septemba 30, 2021.
“Maandalizi yote kuelekea mashindano haya yamekamilika, kesho ni siku yenu kuonesha vipaji, sisi kazi yetu ni kushangilia na mshindi atapatikana kwa taratibu za mashindano haya, akitokea umeshindwa sawa, kwani asiyependa kushindwa si mshindani” amesema Dkt. Abbasi.
Hii ni fursa adhimu kwa nchi yetu kujitangaza kimataifa kutokana na umaalumu wa kundi hili na hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa Serikali imekuwa na mikakati kabambe ya kuinua michezo mbalimbali bila kujali changamoto zao za kimaumbile au jinsia.
Jumla ya washiriki 55 tayari wapo kambini wanaendelea na maandalizi ya mashindano kutoka zaidi ya nchi 13 pamoja na waamuzi kutoka Marekani na Ufaransa. Nchi za Afrika ambao washiriki wake wamefika ni wenyeji Tanzania, Botswana, Burundi, Kenya, Msumbiji, Rwanda, Senegal, Sierra Leone, Sudan Kusini, Uganda na Zimbabwe.
Mashindano haya yanaandaliwa na kuratibiwa na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na Kituo cha Sanaa Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA) yakihusisha vijana wa kike na wa kiume ambao tayari wamewasili jijini Dar es Salaam kujiunga na kambi ya maandalizi kuelekea mashindano hayo kuanzia Septemba 24 hadi 30, 2021.
Mashindano ya dunia yanatarajiwa kufanyika Aprili 2022 ambapo hadi sasa nchi za Brazil na Italia zinapendekezwa kuandaa mashindano hayo.