Na Dotto Mwaibale, Singida.
MWAKILISHI kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Jamii na Lishe, Dinah Atinda amewapongeza wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya ya Singida DC kwa kuwa na uelewa mpana wa uhamasishaji wa chanjo ya Uviko 19 ambao unaendelea nchini kote.
Atinda alitoa pongezi hizo jana kwa niaba ya wenzake katika semina ya siku moja iliyokuwa ikitolewa kwa wajumbe hao wilayani humo.
” Tunapita katika Halmashauri zote kuangalia namna kinavyofanyankazi hiki kikao cha PHC lakini napenda kusema kikao hiki ni tofauti kidogo na vikao tulivyo vipitia ndugu mwenyekiti wa kikao ‘Mkuu wa wilaya’ inaonekana wajumbe wa kikao hiki wamepata elimu ya kutosha na wapo vizuri kabisa hivyo tunawapongeza sana,”. alisema Atinda.
Alisema Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na TAMISEMI na wadau mbalimbali baada ya kuona hali ya nchi sio nzuri ugonjwa wa Uviko 19 unaendelea na watu wanakufa tukaona kuna haja ya kuanzisha mpango mkakati shirikishi na harakishi kwa ajili ya kuhamasisha na kuelimisha jamii ili wote waweze kupata chanjo na kupunguza madhara yanayotokana na ugonjwa huo.
Alisema zoezi la mtu kuchanja ni la hiyari hivyo lifuate maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa vituo vya chanjo sasa vimeongezwa hadi kufikia zaidi ya 6,500 na vinatoa huduma.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Paskas Muragili alisema changamoto kubwa iliyopo kwa Watanzania ni kuwa hawajapewa elimu ya kutosha kuhusu chanjo na hawajui umuhimu wa chanjo hiyo lakini wanauelewa mkubwa wa mambo mbalimbali hivyo ni wajibu wa kamati hiyo kwenda kuwaelimisha na wakielewa watachanja.
Wakizungumza baada ya kupata mafunzo hayo wajumbe wa kamati hiyo walisema sasa wanakwenda kufanya uhamasishaji wa nguvu wakianzia kwenye familia zao.
Walisema uhamasishaji huo wataufanya kwenye nyumba za ibada, magulio, mashuleni, na kwenye mikusanyiko ya watu.
Wajumbe hao walisema wataenda kutoa elimu hiyo kwa viongozi mbalimbali wa vijiji wakiwemo wa Serikali na vyama vya siasa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wana elewa na kujitokeza kwa wingi kwenda kupata chanjo hiyo.