Dar es Salaam –
Shirika Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani la Peace Corps, limesherehekea miaka 60 toka kuwasili kwa wafanyakazi wake wa kujitolea wa kwanza nchini Tanzania kwa hafla fupi iliyofanyika jana jioni na kuhudhuriwa na mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Liberata Mulamula.
Katika hotuba yake, Waziri Mulamula alisema kuwa madhimisho haya ya miaka 60 ya kuwasili kwa Wafanyakazi wa kwanza wa Kujitolea wa Peace Corps ni kielelezo na hatua muhimu katika ushirikiano kati ya serikali na watu wa Marekani na serikali na watu wa Tanzania.
“Maadhimisho ya leo yanadhihirisha hatua nyingine muhimu katika uhusiano rasmi, wa kihistoria na kirafiki baina ya nchi zetu,” alisema Mulamula.
Rais wa Marekani John F. Kennedy alianzisha Peace Corps mwaka 1961, akiwapa changamoto vijana wa Kimarekani kuhudumia wanadamu wengine kwa kufanya kazi kwa ajili ya amani na maendeleo katika nchi nyingine duniani kote. Kwa sababu ya urafiki wa karibu kati ya Kennedy na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania (wakati huo ikiitwa Tanganyika) ilichaguliwa kuwa miongoni mwa nchi za kwanza kabisa duniani kupokea Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps. Tarehe 29 Septemba 1961, Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps wapatao 50 waliwasili mjini Arusha, Tanzania.
Toka wakati huo, takriban Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps wapatao 3,200 wamefanya kazi sambamba na wenzao wa Kitanzania katika mikoa 22 nchini, wakifuta ufumbuzi utokanao na jamii zao, kutanzua changamoto katika elimu, afya, kilimo, mazingira na maendeleo ya vijana.
Kwa mujibu wa Waziri Mulamula, wafanyakazi hawa wa kujitolea wamechangia pakubwa katika maendeleo ya Tanzania.
“Tunatoa shukrani kwa Wamarekani waliofanya kazi bila kuchoka na wafanyakazi wenzao wa Kitanzania katika maeneo ya vijijini kabisa katika nchi yetu wakiwa walimu wa hesabu na sayansi katika shule za sekondari, wakufunzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano, viongozi katika miradi ya kutoa elimu ya afya kwa umma na viongozi katika miradi ya mazingira inayolenga kukidhi mahitaji ya msingi kabisa katika ngazi ya kijiji ya usimamizi endelevu wa maliasili. Shukrani ziwaendee viongozi wetu wenye maono, Mwalimu Nyerere na rais John F. Kennedy wa Marekani kuwezesha program hii kuwepo,” alisema Mulamula.
Katika hotuba yake, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright alisisitiza kuwa Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps wahaohudumu nchini Tanzania nao pia wamepata mabadiliko chanya kutokana na uzoefu wao huo.
“Baada ya miaka miwili ya kufanya kazi bega kwa bega na wenzao wa Kitanzania, wakila pamoja, wakicheka na kujifunza utamaduni wa kila mmoja wao, wafanyakazi wa kujitolea hubadilika milele na huibeba Tanzania mioyoni mwao popote waendapo,” alisema Balozi Wright.
Aidha, Balozi Wright alitoa shukrani kwa serikali na watu wa Tanzania kwa kuisaidia programu ya Peace Corps katika miongo sita iliyopita.
“Kwa dhati kabisa ninapenda kuwashukuru watu wa Tanzania na Serikali katika ngazi zote kwa msaada mkubwa uliotolewa kwa programu na wafanyakazi wa kujitolea katika miaka hii yote. Ninapenda pia kuzishukuru familia na jamii zilizowapokea na kuishi na wafanyakazi wa kujitolea kwa miaka hii yote. Ni kwa sababu yenu, Wafanyakazi wa kujitolewa waliweza kujifunza kikamilifu na kunufaika na utamaduni na ukarimu wa Kitanzania,” alisema.
Kutokana na changamoto zilizojitokeza kutokana na janga la kidunia la UVIKO 19, hivi sasa hakuna Mfanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps anayehudumu nchini. Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps nchini Tanzania, Stephanie Joseph de Goes alisema kuwa ana matumaini kuwa wafanyakazi wa kujitolea watarejea mwaka 2022.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Kitengo cha Habari cha Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa barua pepe: [email protected]