Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani (katikati) akifungua kikao leo cha kupokea taarifa ya robo ya tatu ya Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki
Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt. Yahya Nawanda akitoa maoni yake leo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya robo ya tatu ya Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wadau leo baada ya kumalizika kwa kikao leo cha kupokea taarifa ya robo ya tatu ya Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki
Picha na Tiganya Vincent
*******************************
NA TIGANYA VINCENT
VIONGOZI wa Wilaya za Nzega na Igunga kuanza kuwajengea uwezo Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo katika maeneo yao ili waweze kushiriki kikamilifu katika uendeshaji wa shughuli zao kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi utakaonza hivi karibuni.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya robo ya tatu ya mradi wa bomba la mafuta ghafi.
Amesema ni lazima viongozi hao wajitahidi kutoa elimu kwa ajili ya wajarisiamali na wafanyabiashara ambao ni wadogo waweze kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa ili nao waweze kunufaika na uwepo wa mradi.
Balozi Dkt.Batilda amesema fursa imeshakuja ni jukumu la kila Kiongozi wa maeneo ambayo Kambi zitajengwa na pale Mkuza wa Bomba la Mafuta ghafi utakapopita kuwandaa watu wake kwa ajili ya kushiriki katika kutafuta kipato halali.
Amesema waweke vigezo ambavyo vitasaidia kuonyesha faida zitatokana na ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi
Balozi Dkt.Batilda amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikisisitiza utoaji kipaumbele wa wazawa katika miradi(local Content) kwa lengo la kuwanyanyua na kuboresha uchumi wao nao ni vema wakazingatia hilo.
Amesema suala hilo ni pamoja Wajenzi wa Mradi huo watumiea bidhaa kama mchicha, mchele, kuku, nyama ya ng’ombe kutoka maeneo husika na sio nje ya hapo.
Balozi Dkt.Batilda amesema sanjari na kuwajengea uwezo ni pamoja kuwafundisha namna nzuri ya kufungasha bidhaa zao ili ziwe na ubora na thamani kubwa sokoni.
“Tunao mchele mzuri kutoka katika eneo la Mwanzugi na maeneo mengine ya Nzega…tunao ng’ombe wengi na hivi sasa tunahamasisha ufugaji wa kuku…tuna uhakika wakutoa huduma kwa wageni watakaokuwa wakijenga mradi bila wasiwasi” amesisitiza.
Aidha Balozi Dkt.Batilda ameupongeza utaratibu uliotekelezwa na uongozi wa Mradi Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki wakati wa zoezi la kulipa fidia wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa Kambi na Kiwanda.
Amesema utaratibu huo umesaidia pande zote kufikia muafaka bila mvutano.
Balozi Dkt.Batilda ameutaka Mradi huo kuhakikisha unaendeleza utaratibu huo wa ulipaji fidia katika maeneo ambapo utajengwa mkuza wa bomba la mafuta ghafi.
Amesema kwa watakaotaka fedha wapewe , kwa wale watakaotaka kujengewa nyumba wajengewe na watakaotaka wape ardhi mbadala nao wafanyiwe hivyo ili waweze kuondoka wakiwa na furaha miyoni mwao.