Diwani wa kata ya Liuli Wilayani Nyasa mh.Bonifasi Sangana akipatiwa chanjo ya UVIKO 19 na Muuguzi Msaidizi Thereza Joseph katika Fukwe za,Mbamba bay ziwa Nyasa.Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imewataka watoa huduma kuwahamasisha wananchi kwa kuwafuata maeneo mbalimbali na kuwapa huduma hiyo.na picha nyingine ni watoa Huduma za Chanjo ya Uviko 19 wakitoa elimu kwa wachuuzi wa dagaa Nyasa ili wawaweze kupatiwa chanjo hizo,Picha na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa
**********************************
Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Imekamilisha zoezi la kutoa mafunzo kwa watoa Huduma ya kuchanja, Chanjo ya UVIKO 19 katika vituo vyote vya kutolea huduma ya Afya Wilayani hapa.
Lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wataalam hao, ili waweze kutoa chanjo kwa wananchi wote wa Wilaya ya Nyasa, ili kupunguza Mnyororo wa kujikinga na ugonjwa wa UVIKO19
Mganga mkuu wa Hamashauri ya wilaya ya Nyasa Deus Ruta,amesema tayari Halmashauri imetoa mafunzo kwa watoa Huduma za Afya kwa tarafa 3 za wilaya ya Nyasa, Ambazo ni Ruhekei, Mpepo, na Ruhuhu, na lengo ni kuwafikia, kutoa chanjo kwa wananchi wa wilaya ya nyasa, ili wananchi wawe na uhakika wa afya na kujikinga na ugonjwa wa UVIKO19.
Ameongeza kuwa mpango wa serikali, ni kuhakikisha chanjo inawafikia wananchi wote na kutoa Elimu kwa wananchi wote ili wapate chanjo ambayo inatolewa bure na Serikali itahakikisha inatoa elimu na kuwahamasisha wananchi kupata chanjo hiyo ambayo ni muhimu ili kuweza kuukabili ugonjwa huu.
“Wilaya ya Nyasa tumejipanga kuhakikisha kuwa chanjo hii inamfikia kila mwanachi mwenye uhitaji wa kuchanja na tunatoa elimu kwa wananchi ili waweze kupata uelewa na wito wangu kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuhakikisha wanachangamkia fusa ya kuchanja kwa kuwa chanjo hiyo hutolewa bure” alisema.
Wito kwa wananchi wa wilaya ya nyasa kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hiyo kwa kuwa inatolewa bure na imesogezwa katika kila kituo cha kutolea huduma ya Afya.
Kwa upande wao washiriki mafunzo wamesema watafanya kazi kwa bidii ya kutoa elimu, kuhamasisha jamii kupata chanjo hii na kuchanja ili kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora.