…………………………………………………………….
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma, Deo Ndejembi amefanikisha upatikanaji wa kiasi cha Sh Milioni 103 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa manne na matundu 10 ya vyoo kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kata ya Zajilwa.
Kiasi hicho cha fedha kitakamilisha ujenzi wa Madarasa hayo pamoja na samani zake kwa maana ya madawati na ambapo pia matundu hayo 10 nane yatakua ya wanafunzi na mawili ya walimu.
Ndejembi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Zajilwa akiwa kwenye ziara yake ya kuzungumza na wananchi ambapo amewahakikishia kuwa ukamilishaji wa umeme kwa baadhi ya vijiji vya Kata hiyo utaanza Oktoba mwaka huu.
“Nichukue fursa hii kwa niaba yenu kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa TASAF kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha hizi ambazo zitakwenda kukamilisha madarasa haya manne, matundu 10 ya vyoo na haya madarasa siyo majengo tu yatakua na Viti na Meza, haya yote nimefanya kama Mbunge wenu kuwatua mzigo wa kuchangishana kila siku kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari.
Kupitia fedha hizi tunakwenda kukamilisha ujenzi wa Shule hii ambayo niliahidi kipindi cha kampeni na sasa tunatekeleza, hii ndio kazi ambayo niliwaomba na ni lazima niitekeleze kwa nguvu na kasi,” Amesema Ndejembi.
Kuhusu changamoto ya miundombinu ambayo kwa kipindi kirefu imekuepo kwenye Kata hiyo, Ndejembi amesema tayari washapokea Sh Bilioni 1.5 kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya Barabara hivyo fedha hizo zimeshafika kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Wilaya ya Chamwino na tayari mkandarasi ameshaanza kazi.
“Kipekee nimpongeze Rais Samia kwa kutupatia kiasi hicho cha fedha ambacho alitoa kwa majimbo yote nchini, hivyo Mimi baada ya TARURA kunishirikisha nikasema sasa ni wakati Tarafa hii ya Itiso ambayo Zajilwa Iko ndani yake kumaliza changamoto hiyo ya Barabara.
Kwa kusema hivyo tayari mkandarasi yupo kazini tunaanza kutengeneza njia panda,itapita hapa Zajilwa kuelekea Gwandi na kutokea Haneti ni Barabara nzuri ambayo itapitika kwa nyakati zote haya yote ni matokeo ya fedha ambazo tumepatiwa na Rais wetu Samia tunamshukuru sana,” Amesema Ndejembi.