Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza kwa na waombolezaji mara baada ya kukamilika kwa ibada ya kumuaga aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji William Ole Nasha katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma. Septemba 30, 2021.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwafariji wana familia ya marehemu William Ole Nasha aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa Ole Nasha iliofanyika katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma (Septemba 30,2021)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango na mkewe mama Mbonimpaye Mpango wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji , William Ole Nasha shughuli iliofanyika katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma (Septemba 30,2021)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wakishiriki Ibada ya kumuaga aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji marehemu William Ole Nasha katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma. Septemba 30, 2021
Mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji marehemu William Ole Nasha ukiwasili katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma kwaajili ya Ibada na shughuli ya kuaga mwili huo. Septemba 30,2021.
*******************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ameshiriki ibada na baadaye shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji marehemu William Tate Olenasha iliofanyika katika viwanja vya Bunge la Jamuri ya Muungano wa Tanzania septemba 30, 2021.
Shughuli ya kuaga mwili wa Marehemu William Ole Nasha imeongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge, Dini, viongozi wa Ulinzi na Usalama pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais ametoa pole kwa wote walioguswa na msiba wa Ole Nasha na kuwaomba kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika wakati huu mgumu.
Amesema marehemu Ole Nasha alitumia taaluma yake vizuri kuleta maendeleo kwa taifa na kuwatumikia wananchi wake wa Ngorongoro kwa moyo wake wote. Makamu wa Rais amemtaja marehemu Ole Nasha kama kiongozi alikuwa mchapakazi na mzalendo kwa nchi yake.
Aidha Makamu wa Rais amesema Marehemu Ole Nasha atakumbukwa kwa msaada wake aliokuwa akiutoa kama Naibu Waziri katika masuala mbalimbali bungeni ikiwemo mchango wake katika kutetea muswada wa sheria ya fedha.
Awali Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai amemtaja marehemu William Ole Nasha kama kiongozi aliyeamua kusoma sheria ili kuondoa changamoto zinazokabili jamii inayomzunguka ya wana Ngorongoro. Amesema Bunge limempoteza mbunge alikuwa makini na mwaminifu katika kuwatumikia wananchi wake.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema marehemu Ole Nasha atakumbukwa kwa kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa weledi hapa nchini na kuaminiwa kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Amesema Ole Nasha kwa kutumia taaluma yake ya sheria amefanya kazi ya kutuliza migogoro mingi ya uwekezaji iliokuwepo hapa nchini.