Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Mbaraka Batenga
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Mrakibu mwandamizi wa uhamiaji (SSI) Mbaraka Batenga, amewataka wananchi kuachana na habari potofu zinazotolewa kwenye mitandao ya kijami juu ya chanjo ya Uviko-19.
Batenga akielezea mikakati ya wilaya hiyo katika kuhakikisha chanjo hiyo inasambazwa maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo amewataka wananchi kuchanja kwani Uviko-19 unaua hivyo waachane na habari potofu za mitandao
Amesema chanjo ipo na watu wanapaswa kurudi kwenye utafiti wa kisayansi kuliko kutegemea habari potofu za mitandao ya kijamii hivyo watu wakapate chanjo ya Uviko-19.
Amesema mikakati yao ni mikubwa katika kuhakikisha chanjo inapatikana kwani zimesambazwa maeneo mbalimbali ya zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya.
“Kiteto kuna vijiji 63 na tuna zahanati 27 bado hazijatosheleza kwani kuna umbali kutoka sehemu moja kwenda na baada ya kubaini hilo tumeandaa timu ya kutembea (mobile) kwa lengo la kuwafikia wote na kuwachanja,” amesema.
Amesema wataalamu wa afya wanawafuata watu kwenye maeneo yao na kutoa elimu na wenye kuelewa wanapatiwa chanjo hiyo ambayo wengine wanatembea nayo kwani siyo ajabu hata kina mama huwa wanapata huduma ya mobile clinic.
“Tathimini yetu ni kuwa kila kwenye mobile wanapata matokeo chanya kenye chanjo hii kwani wananchi wanaelewesha na kuchanja,” amesema Batanga.
Amesema makundi ya pembezoni wakiwemo jamii ya wandorobo nao watapatiwa chanjo hiyo kwa kufikiwa kwenye maeneo yao ili kuhakikisha wote wanaohitaji wanachanjwa.
“Kimsingi tumewagawa watu katika makundi yote na tutawafikia hata watu waliopo kwenye taasisi mbalimbali tunawafikia ikiwemo za elimu, kwenye benki, magereza na taasisi nyingine,” amesma Batanga.
Mkazi wa kata ya Kibaya, Hashim Juma amesema baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha kwenye mitandao ya kijamii kuwa mtu akipatiwa chanjo ya Uviko-19 anageuka kuwa zombie.
“Watu hawana elimu ya Uviko-19 ila wanatangaza mambo ambayo hawana uhakika nao, mimi binafsi nimechanja na sikupata madhara yoyote,” amesema Juma.
Amesema endapo mtu akipata ndugu, jamaa au rafiki aliyewahi kuugua Uviko-19 na kufariki dunia au akapona hawezi kusita kupatiwa chanjo ya Uviko-19.
Mwalimu wa shule ya msingi Bwagamoyo John Mollel amesema wataalamu wa afya wanapaswa kuendelea kutoa elimu ya Uviko-19 ili watu wanaoendelea kupotosha kwenye mitandao waache.
Mollel amesema baadhi ya watanzania hanawa utaalamu wa afya ila wanaongeza chumvi kwa jambo ambalo hawana uhakika nao suala ambalo siyo sahihi.