Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (mstaafu) Mhe. Dkt. Steven J. Bwana (kushoto) akisalimiana na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Modest Kirama, baada ya kufika katika Ofisi ya Tume iliyopo Jengo la Chimwaga, Jijini Dodoma leo tarehe 28/09/2021.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Modest Kirama (kulia) akipokelewa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (mstaafu) Mhe. Dkt. Steven J. Bwan, baada ya kufika Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma iliyopo Jengo la Chimwaga, Jijini Dodoma, kushoto ni Bw. John C. Mbisso, Naibu Katibu wa Tume.
Bw. John C. Mbisso (kushoto) Naibu Katibu wa Tume, akifafanua jambo kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama (katikati) baada ya Katibu wa Tume kufika Ofisi ya Tume, Chimwaga Dodoma leo 28/09/2021. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (mstaafu) Mhe. Dkt. Steven J. Bwana.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama (wa nne kutoka kulia) katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji (mstaafu) Dkt. Steven J. Bwana (wa tano kutoka kulia) na baadhi ya watumishi wa Tume, baada ya Katibu kufika katika Ofisi ya Tume Chimwaga- Dodoma, leo 28/09/2021.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama akipokelewa baada ya kuwasili katika Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma, Chimwaga – Dodoma, leo tarehe 28/09/2021.
*******************************
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bwana Mathew Modest Kirama amewataka watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma kuongeza kasi ya utendaji wa kazi ili kufikia malengo yaliyowekwa na Tume.
Bwana Kirama aliapishwa jana tarehe 27 Septemba 2021 na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, amesema haya leo baada ya kufika Ofisini kwake, Ofisi ya Tume iliyopo katika Jengo la Chimwaga, Dodoma na kupokelewa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Jaji (mstaafu) Mheshimiwa Dkt. Steven James Bwana, Wakuu wa Idara na Vitengo na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma.
“Tume ya Utumishi wa Umma ina jukumu la kuhakikisha Waajiri, Mamlaka za Ajira, Mamlaka za Nidhamu na Watumishi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali, ninapenda kila mmoja katika nafasi yake ahakikishe anawajibika ipasavyo, anajitoa kadri anavyoweza kuhakikisha tunafikia malengo ya Tume. Mahali tunapofanya vizuri, tuhakikishe tunazidi kufanya vizuri zaidi. Ongezeni kasi ya utendaji wa kazi. Nafahamu Tume kuna changamoto, kwa pamoja tunapaswa kushirikiana ili kutafuta majawabu ya changamoto hizo” amesema Bwana Kirama.
Bwana Mathew Kirama amewapongeza na kusisitiza uwajibikaji zaidi Watumishi wa Tume kwa namna ambavyo kila mmoja anavyojitoa wakati wa kutekeleza majukumu yake pamoja na changamoto zilizopo kuhakikisha majukumu ya Tume hasa yale ya kisheria ya kushughulikia rufaa na malalamiko na Ukaguzi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma yanaendelea kufanyika.
Akizungumzia umuhimu wa kutatua kero za watumishi wa Tume, Bwana Kirama amesema ni muhimu Wakuu wa Idara na Vitengo wa Tume kutenga muda wa kukutana na kusikiliza kero na matatizo ya watumishi walio chini yao na kutafutia ufumbuzi.
“Tunapaswa kuendelea kuanzia pale mtangulizi wangu alipoishia, unahitajika utashi wa kila mmoja wetu, kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, ushirikiano, maelewano, kuheshimina na kutambua nafasi na mchango wa kila mmoja ili kufanikisha malengo ya Tume” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (mstaafu) Mheshimiwa Dkt. Steven James Bwana amempongeza Bwana Kirama kwa kuteuliwa na kuapishwa kuwa Katibu wa Tume.
“Nina matumaini makubwa sana kwako Katibu wa Tume, Mathew Kirama naamini ni mtu sahihi na huu ni wakati sahihi kwako kuiongoza Tume ya Utumishi wa Umma. Nawaomba watumishi wa Tume kutoa ushirikino mkubwa kwako Katibu ili uweze kuifikisha Tume katika malengo yake iliyojiwekea” amesema Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bwana Mathew Modest Kirama ameteuliwa na kuapishwa na Mheshimiwa Rais, kuchukua nafasi ya Bwana Nyakimura Muhoji ambaye amestaafu.