***************************
NJOMBE
Mkoa wa Njombe unatajwa kuwa kitivo cha kilimo cha Parachichi kufuatia uwekezaji mkubwa na wakuridhisha ambao umekuwa kivutio kwa wakulima kutoka mikoa mingine hapa nchini.
Hayo yalisemwa na meneja mkuu wa maendeleo kutoka shirika la TAHA Anthony Chamanga wakati wa mafunzo kwa wakulima wa Parachichi ya kuwasaidia kuongeza mavuno na tija ambayo yamefanyika mkoani Njombe na kuhudhuriwa na wakulima kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Njombe.
Alisema lengo la kufanya mafunzo hayo mkoani hapa ni kwasababu mkoa huo unaelekea kuwa kitivo cha uzalishaji wa zao la Parachichi hapa nchini.
Alisema pia mafunzo hayo yamefanyika mkoani Njombe ili wakulima kutoka mikoa mingine waweze kuzifahamu mbinu zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji.
Alisema mkoa wa Njombe una mazingira tofauti ukilinganisha na mikoa mingine katika suala zima la uzalishaji wa Parachichi.
“Mafunzo yetu yanahusisha wakulima wa Parachichi kutoka mikoa mitatu ambayo ni Arusha, Manyara lakini pia hapa Njombe na kwa ujumla tutakuwa na washiriki zaidi ya 120” alisema Chamanga.
Alisema kupata mavuno kidogo katika zao la Parachichi ni changamoto ya muda mrefu ambayo imekuwa kizuizi kwa mkulima kufikia uzalishaji mkubwa utakaomuwezesha kupata mapato ya kutosha.
Alisema katika hali ya kawaida mche mmoja wa Parachichi unaweza kutoa kilo 150 lakini wakulima wengi wanapata katika ya kilo 30 hadi 50 ambapo upotevu wa mazao ukiwa mkubwa zaidi kati ya asilimia 40 hadi 50.
Akitoa mafunzo hayo mara baada ya wakulima hao kutembelea shamba darasa ili kujifunza kilimo hicho cha Parachichi bwana shamba kutoka mtaa wa Maheve kata ya Ramadhani Tito Mng”ong’o alisema shamba hilo kwa wastani linatoa tani 12.5 za Parachichi kwa mwaka ambapo kwasasa kilo moja ya Parachichi inauzwa 1650.
Alisema Parachichi ni zao ambalo linahitaji maji kwa wingi pamoja na mbolea ya kutosha ya samadi hivyo mkulima anapaswa kutilia mkazo ili kuweza kupata mavuno ya uhakika.
“Tangu mwaka 2014 hadi mwaka huu shamba hili tumeweza kuchuma tani 13 za Parachichi sasa ukizidisha kwa bei tunayouza kilo moja shilingi 1650 utaona kiasi cha fedha kinachopatikana” alisema Mng’ong’o.
Mwenyekiti wa kongani ya Parachichi mkoa wa Arusha Elishilia Ayo alisema lengo la kufika mkoani Njombe ni kujifunza namna ambavyo wakulima mkoani hapa walivyoweza kupandisha uchumi wa mkoa huo kupitia kilimo cha zao la Parachichi.
Alisema kitendo hicho kimewafanya kutamani kujifunza mbinu walizotumia wakulima wa Parachichi mkoani Njombe kwa kushirikiana na TAHA ambao wamewawezesha kufika mkoani hapa.
“Njombe siyo mamilionea bali ni mabilionea kwani tumekutana na mtu anaitwa shikamoo Parachichi ambae alianza chini sana lakini sasa hivi ni moja ya mabilionea wa nchi hii” alisema Ayo.
Baadhi ya wakulima walioshiriki mafunzo hayo kutoka mikoa hiyo wakiwemo Erasto Ngolle na Rogate Ayo walilishukuru shirika la TAHA kwa kuandaa mafunzo hayo kwani wanaamini yamewajengea uwezo mkubwa na kuahidi kufanyia mafunzo waliyopata ili kilimo hicho kiwe na tija.
“TAHA walipofika shambani kwangu ni kweli walikuta shamba la Parachichi kati ya miche 116 iliyokuwepo ni mche mmoja pekee uliokuwa na uwezo wa kutoa Parachichi inayoweza kupata soko la kimataifa” alisema Ngolle.