…………………………………………………………………………
NA TIGANYA VINCENT
MKUU wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani ametoa elimu kwa wakazi wa Kijiji cha Mwisole wilayani Uyui kuhusu umuhimu wa kupata chanjo ya UVIKO 19 na kufanya watu kujitokeza na kupata chanjo katika eneo la Mnada wa Mwisole.
Dkt. Batilda ameendesha zoezi hilo leo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kufikisha elimu kwa wananchi wengi ambao bado hawana uelewa sahihi wa faida ya chanjo ya UVIKO 19.
Amesema viongozi wa Kitaifa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wameshachanja na wale wa Mkoa wa Tabora na wameshachanjwa na hakuna madhara yoyote waliyopata.
Dkt. Batilda chanjo hiyo salama na inatolewa bure kwa mwananchi yoyote ambayo umri wake unazidi miaka 18 .
“Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anatupenda sana na ndio maana ametuletea chanjo kwa ajili ya kupambana na ugonjwa UVIKO 19 ambao ni hatari sana …ni vema kwa wale ambao hawajachanjwa wakachangamkia fursa hiyo…na hivi sasa hatuki mfuate chanjo mbali tunawaletea huku mlipo” amesisitiza
Dkt. Batilda amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan inajari sana afya za wananchi wake na ndio maana inajenga miundombinu mbalimbali ambao kwa Mkoa wa Tabora imetoa fedha kwa ajili ya kuongeza Vituo vya Afya vipya viwili.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo amewakumbusha wakazi wa Tabora kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19 kwa kuepuka misongamano,kunawa na maji tiririka na kuvaa barakoa.