Mstahiki Meya wa halmashauri ya Manispaa Tabora Ramadhan Shaban Kapela (aliyesimama) akiongea na Waheshimiwa Madiwani jana katika kikao maalumu cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa manispaa mjini Tabora. Picha na Lucas Raphael,Tabora
**********************************
Na Lucas Raphael,Tabora
MADIWANI wa halmashauri ya Manispaa Tabora wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuliwakilisha vyema taifa katika Baraza la Umoja wa Mataifa na kuudhihirishia ulimwengu juu ya maono yake makubwa ya kimaendeleo.
Rai hiyo ilitolewa katika kikao maalumu cha baraza la madiwani kilichofanyika jana katika ukumbi wa manispaa ambapo wamewataka wadau wa maendeleo kumuunga mkono ili aweze kutimiza maono makubwa aliyonayo.
Walisema kuwa hotuba aliyotoa hivi karibuni katika Mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa nchini Marekani imeliletea heshima kubwa taifa na imeonesha jinsi alivyo na upeo mpana na maono makubwa ya kimaendeleo kwa taifa lake na dunia kwa ujumla.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Shaban Kapela alisema kuwa Rais Samia licha ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Urais katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni jasiri na ana uwezo mkubwa wa uongozi.
Alibainisha kuwa ushauri aliotoa mbele ya Viongozi wa Umoja wa Mataifa (UN) na Wakuu wa nchi umeonesha jinsi alivyo na ndoto kubwa za maendeleo endelevu na anavyotamani kuona mataifa makubwa yakishirikiana ipasavyo na nchi ndogo hivyo anapaswa kuungwa mkono.
‘Tunampogeza sana mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutuwakilisha vyema katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa, hakika tumepata kiongozi shupavu mwenye maono makubwa ya kimaendeleo, dunia sasa inatutambua’, alisema.
Mstahiki Meya aliwataka viongozi na watendaji wote wa serikali kuendelea kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kuhakikisha miradi yote inayoanzishwa na serikali ya awamu ya sita inakamilika kwa wakati na kunufaisha wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tabora Dkt Yahaya Nawanda alibainisha kuwa Rais Samia amedhihirisha kipaji na uwezo mkubwa aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika suala zima la uongozi.
Alifafanua kuwa Rais amefanya mambo makubwa sana katika kipindi kifupi tu cha uongozi wake, hivyo akasisitiza umuhimu wa kila mtu kuchapa kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi hizo.