Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Viongozi wa Wizara na Wajumbe wa Benki ya Dunia waliongozwa na Makamu wa Rais wa Benki hiyo Dkt. Hafez Ghanem (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam kilichojadili utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Viongozi wa Wizara na Ujumbe wa Benki ya Dunia (hawapo pichani) ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Benki hiyo Dkt. Hafez Ghanem. Kikao hicho kimefanyika Jijini Dar es Salaam ambapo wamejadili utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu inayofadhiliwa na Benki hiyo.
Viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Benki hiyo Dkt. Hafez Ghanem wakiwa kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem wakisalimiana kabla ya kuanza kwa kikao cha viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ujumbe wa Benki ya Dunia kilichofanyika jijini Dar es Salaam
…………………………………………………………
Serikali imesema itahakikisha fedha zinazotolewa na wadau wa maendeleo kwa ajili ya miradi ya Sekta ya Elimu zinatumika kwa kazi zilizopangwa huku mkazo ukiwa katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia elimu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alipofanya kikao jijini Dar es Salaam na ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Makamu wa Rais wa Benki hiyo Dkt. Hafez Ghanem ambapo amesema benki hiyo inafadhili miradi mikubwa mitano katika sekta ya elimu.
Waziri Ndalichako ameitaja miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo kuwa ni pamoja na Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) (unafadhiliwa kwa ushirikiano na FDCO, SIDA, KOICA na GPE),Mradi wa Kukuza na Kuendeleza Ujuzi (ESPJ), Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Uchumi (HEET), Mradi wa Kuongeza Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na Mradi wa Afrika Mashari wa Kuboresha Mafunzo ya Ufundi (EASTRIP) ambayo utekelezaji wa miradi hiyo uko katika hatua mbalimbali.
“Serikali ya Tanzania inashukuru kwa ufadhili wa Miradi ya sekta ya Elimu ambao umetolewa na Benki ya Dunia. Utekelezaji wa Miradi hii umeleta mafanikio katika ngazi zote za elimu ikiwemo ongezeko la fursa za elimu ikiwa ni matokeo ya uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia, upatikanaji vifaa, uboreshaji wa mbinu za ufundishaji, huduma za maji salama na safi shuleni, ongezeko la walimukupelekwa katika shule nchini (teacher deployment) na uimarishaji uthibiti Ubora wa Shule” amesema Profesa Ndalichako.
Ndalichako ameongeza kuwa utekelezaji wa Miradi hiyo umewezesha ongezeko katika uandikashaji katika shule za msingi kutoka 93% mwaka 2020 hadi 95.3% mwaka 2021 wakati katika ngazi ya sekondari ongezeko ni 35% mwaka 2020 hadi kufikia 37% mwaka 2021.
Aidha, kupitia Mradi wa SEQUIP Ndalichako amesema tayari serikali imepokea takribani Dola milioni 74 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya za sekondari ambazo zinatarajiwa kuchukua wanafunzi zaidi ya 300,000. Mradi huu pia utasaidia wanafunzi wa kike zaidi milioni 3.1 kupitia shule maalum zitakazojengwa za wasichana na vituo maalum vitakazoimarishwa kwa ajili ya kutoa elimu kwa njia mbadala kwa wanafunzi waliopata mdondoko.
Akizungumzia namna utekelezaji wa miradi hiyo ilivyoongeza ufaulu, Profesa Ndalichako amesema kumekuwa na ongezeko la ufaulu kutoka 79.4% mwaka 2019 hadi kufikia 82.7% mwaka 2020 kwa shule za msingi, wakati kwa upande wa sekondari kidato cha nne ufaulu umeongezeka kutoka 80.65% mwaka 2019 hadi 85.8 mwaka 2020.
Kwa upande wa kuendeleza ujuzi kupitia mradi wa kuendeleza ujuzi (ESPJ) amesema kumekuwa na uboreshaji na kuongeza miundombinu ya ufundishaji na kujifunzia katika vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi hali ambayo iimewezesha kuongezeka kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo kutoka 5,520 mwaka 2019/20 hadi kufikia 15,032 mwaka 2020/21 na pia mradi umewezesha ujenzi wa vyuo 29 vya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA).
Wakati huo huo Waziri Ndalichako ameeleza kuwa Serikali na Benki ya Dunia zipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu juu ya mradi mpya wa kuendeleza elimu ya msingi “BOOST Project” ambao pia utafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa Dola za Kimarekani milioni 200. katik majadiliano yaliyofanyika jana wamezungumzia pia kuongeza ufadhili huo kutoka USD miliono 200 hadi Milioni 300.
Naye Makumu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem amesema nia ya Benki ya Dunia ni kuiwezesha Serikali ya Tanzania kufanikisha utekelezaji wa sera ya Elimu ili kuwezesha kila mtoto wa Kitanzania kupata elimumsingi.
Aidha, ameitaka wizara hiyo kuona jinsi ya kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi zote za elimu.