Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia magonjwa yasiyoyakuambukiza wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.James Kihologwe,akizungumza wakati akitoa tamko la siku ya kichaa cha Mbwa kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali leo September 28,2021 jijini Dodoma.
……………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
IMEELEZWA kuwa kati ya asilimia 30 hadi 50 ya waathirika wa ugonjwa wa kichaa cha Mbwa ni watoto chini ya umri wa miaka 15.
Kauli hiyo imetolewa leo September 28,2021 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia magonjwa yasiyoyakuambukiza wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.James Kihologwe,wakati akitoa tamko la siku ya kichaa cha Mbwa kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali.
Dk.Kihologwe amesema kuwa ugonjwa huo unakadiriwa kusabbaisha takribani vifo 59,000 Duniani ambapo inakadiriwa kuwa silimia 36 ya vifo hivyo hutokea katika bara la Afrika .
“Kama tulivyoona hapo juu kuwa waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto chini ya miaka 15 na hii ni sababu wao ndio wanaokuwa karibu na mbwa muda mwingi na pia hupenda kucheza au kuchokoza mbwa wasiwafahamu njiani,”amesema Dk.Kihologwe
Aidha amebainisha kuwa pamoja na ugonjwa huo kusababisha vifo ugonjwa huo pia husababisha athari kubwa kiuchumi kwani chanjo ambayo ndio njia kuu ya kuzuia mtu kupata ugonjwa ni ya gharama kubwa.
Amesema kuwa Utafiti uliofanyika Mwaka 2002 ulibainisha kuwepo na uwezekano wa takribani vifo 1499 kwa mwaka nchini kutokana na ugonjwa huo.
”Serikali inatambua gharama kubwa za upatikanaji wa chanjo na kupitia Wizara ya Afya,TAMISEMI na sekta nyingine zimechangia gharama za upatikanaji wa chanjo ili ziwafikie wananchi kwa gharama wanayoimudu.’”Amesema Dk.Kihologwe
Hata hivyo amesema kuwa ndani ya miezi nane watu 39,787 wameng’atwa na mbwa ikiwa ni ongezeko la zaidi ya watu 5000 ukilinganisha na kipindi kama hicho cha mwaka uliopita.
Dk.Kihologwe amesema kuwa Mikoa ya Morogoro na Dodoma imeonyesha kuongoza kuwa na matukio hayo ya watu kuumwa na Mbwa au wanyama wa jamii hiyo ambapo Morogoro ni 4,329 na Dodoma ni 4,233.
Hivyo Dk.Kiologwe amesem kuwa katika kudhibiti ugonjwa huo,Wizara ya Afya imekuwa ikishirikiana na Sekta nyingine ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Afya Duniani ili kuhakikisha inapunguza ukubwa wa tatizo hilo pamoja na kutoa elimu.