……………………………………………..
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameishukuru serikali kwa kutoa shilingi Milioni 250 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya katika Tarafa ya Mungaa ambacho kukamilika kwake kitaondoa adha kwa Wananchi ya kutembea umbali mrefu.
Mtaturu ametoa shukrani hizo Septemba 27,2021 katika ziara kwenye kata ya Ntuntu yenye lengo la kuwataarifu wananchi namna serikali ilivyojibu maombi yao.
Amesema serikali imepanga kuwapatia Shilingi Milioni 500 na yatajengwa majengo saba ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje(OPD),Maabara,Jengo la mama na mtoto, chumba Cha kuhifadhia maiti, nyumba ya mganga,jengo la kufulia na kuchomea taka.
“Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita chini ya Mh.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha hizi za kuanzia Ili tuanze ujenzi huu,sote tunajua changamoto iliyokuwepo kutembea umbali mrefu kufuata huduma,na hatua hii itasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto,”alisema.
Akizungumza katika ziara hiyo,diwani wa kata ya Ntuntu Omari Toto ameishukuru serikali na mbunge Mtaturu kwa jitihada za kupeleka fedha ili kujenga Kituo cha afya, Madarasa,maabara na miundombinu ya barabara mambo yaliyokiwa kilio cha muda mrefu sana.
“Tunaishukuru serikali pamoja na mbunge wetu Mtaturu kwa jitihada zilizozaa matunda leo tunajengewa kituo cha afya,hatuamini ni kama ndoto lakini ni kweli serikali yetu sikivu imeendelea kutenda,”alisema.
Katika ziara hiyo Mtaturu amegawa jezi za michezo kwa ajili ya timu za vijiji vyote vitano vya kata ya Ntuntu ikiwa ni maandalizi ya kuanza mtanange wa ligi ya Mtaturu Jimbo Cup itakayotimua vumbi mapema mwezi wa kumi na kushirikisha kata zote 13 zenye vijiji 50.