Na Joseph Lyimo
KIKOSI kazi cha Madhehebu ya Dini mbalimbali chenye wajumbe 22 kimetajwa kuwa mkombozi wa kutoa elimu juu ya Uviko – 19 na kusaidia waumini nchi nzima kuendelea kuabudu kwa uhuru na watu wakiwa salama.
Wajumbe wa kikosi hicho ambao wanatembelea nchi nzima kutoa elimu ya Uviko- 19 na kueleza umuhimu wa chanjo ni maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo (CCT) madaktari wa Kanisa la Kinjili la kilutheri Tanzania (KKKT), Mashekhe kutoka Baraza la kuu la waislam Tanzania (BAKWATA), Rais wa Baraza la maaskofu Tanzania (TEC) na Mufti.
Mkurugenzi wa afya kutoka Kanisa la Kinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) makao makuu Dkt Paul Mmbando amesema wameamua kutoa elimu kwa viongozi wa dini mbalimbali kwa kuwa wanafanya nao kazi kwa ukaribu.
“Lengo la kuwapa elimu hii wafanye ibada zilizo salama waumini na viongozi wa dini wawe salama na waendelee na shughuli zao za kiuchumi,” amesema Dk. Mmbando.
Amesema wameona viongozi hao wa madhehebu ya dini mbalimbali wanaweza kutoa elimu kwa watu wengine wanaowaongoza.
Mtaalamu huyo wa afya amesema kikosi kazi hicho kinatembea nchi nzima kikielimisha watu juu ya umuhimu wa chanjo ya Uviko-19.
Amesema watawafikia viongozi wote kupitia mikutano kwa kutiana moyo na kuelimishana maana chanjo ni sayansi na kuwaelekeza jinsi inavyofanya kazi.
Amesema mafanikio ambayo wameyapata toka kikosi kazi kianzishwe Juni 30 mwaka huu ni kuwa na uhuru wa kuabudu na waumini wakawa salama na kuendelea kupata huduma za kiroho.
“Zaidi ya asilimia 80 ya waumini wa imani mbalimbali ambao wanapata uhuru wa kuabudu kwa kipindi chote hiki cha janga la Uviko-19,” amesema Dkt Mmbando.
Kaimu mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Babati Dkt Emmanuel Mkonyi amesema wameamua kutoa elimu hiyo kwa viongozi wa dini kwa kuwa wana ushawishi na wanaaminika katika jamii.
Dkt Mkonyi amesema mpaka sasa wameishachanjwa watu 1,300 katika Halmashauri hiyo huku akidai chanzo cha watu kutochanjwa wengi ni uelewa mdogo wa wananchi juu ya chanjo ya Uviko-19.
Mchungaji Shedrack Swai wa Kanisa la KKKT Magugu alishauri miili ya watu waliokufa kwa Uviko-19 ikichukuliwa kutoka chumba cha kuhifadhia maiti isiingizwe tena nyumbani badala yake ipelekwe moja kwa moja makaburini kwa ajili ya maziko.
Sheikhe wa wilaya ya Simanjiro Ibrahim Abdallah amesema elimu waliyopewa ni nzuri nao wataishusha kwa waumini wao ili wajikinge na Uviko – 19 na wakachanje.
“Suala la kupatiwa chanjo halina ujanja kwani unakuwa umejikinga na maradhi hayo na hata ikitokea bahati mbaya umeupata hautadhurika sana,” amesema Sheikhe Abdallah.
Paroko msaidizi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu, Padri Elia Kimaro aliwataka waumini wa eneo hilo kuendelea kusali kanisani hapo huku wakichukua tahadhari ya Uviko-19.
Padri Kimaro amesema janga hilo limesababisha waumini kupungua kushiriki kusali kanisani na kuwataka kuendelea kumuomba Mungu na kumtukuza bila hofu.
“Tunaendelea kuchukua tahadhari zilizotolewa na wataalamu wa afya ila tusione kanisani pekee ndiyo tunaweza kupata Uviko-19 na sehemu nyingine hakuna, siyo vyema watu washiriki ibada kanisani,” amesema.
Imamu msaidizi wa taasisi ya Masjid Noor mji mdogo wa Mirerani, Mohamed Shauri alisema viongozi wa dini wameweka wazi msimamo wao juu ya kujikinga na janga la Uviko-19.
Ustaadhi Shauri alisema jambo la mtu kulinda afya yake ni suala la wajibu na ni la lazima kwa sababu afya haina mbadala katika maisha na huwezi kufanya jambo la maana kama hauna afya.
Amesema hata katika maandiko matakatifu ya Mungu ipo aya iliyoweka wazi kabisa mambo ambayo Waislamu hawana hiari nayo ikiwemo suala zima la afya.
“Suala la ulazima wa kulinda afya zetu unapaswa kutiliwa mkazo kwenye wakati huu ambapo hivi sasa dunia nzima inapambana na janga la Uviko-19,” amesema ustaadhi Shauri.