…………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Pwani, kimejipanga kuunga mkono kwa asilimia 100, dhamira ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Samia Suluhu Hassan ya kugombea Urais 2025 na kuhakikisha anashika dola.
Aidha chama hicho kimepongeza hotuba ya kwanza ya Rais Samia aliyoitoa katika mkutano wa 76 kwenye Baraza Kuu la Umoja na Mataifa ambayo imegusa maisha ya watanzania na kulitangaza Taifa kwa uwekezaji na utalii.
Akitoa maazimio manne ya mkutano wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi mkoa ,katibu wa CCM Pwani ,Elias Mpanda alisema dhamira ya kushika dola mwanamke katika uchaguzi mkuu ujao ni wa kuungwa mkono.
Alisema ,wanachama wa CCM wapo sambamba kwa CCM kushinda kwa kishindo ikifika wakati huo.
Pamoja na hilo ,Elias alieleza Rais Samia tangu ameingia madarakani ameendelea kudumisha ushirikiano kimataifa na amethubutu kuongea na wawekezaji na wafanyabiashara na kupanua wigo wa uwekezaji kwa kiwango kikubwa.
Pia wamehimiza wananchi kupata chanjo ya Uviko 19 kwani ni chanjo salama .
Hata hivyo Elias ,aliwataka wananchi kujiandaa na sensa ya watu na makazi 2022 .
Awali Mwenyekiti wa CCM Pwani, Ramadhani Maneno alisisitiza umoja na mshikamano kwa wanaCCM .
Aliipongeza serikali ya awamu ya sita,kwa kuinua uchumi, maendeleo na kudumisha na kuimarisha demokrasia .
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani , Aboubakari Kunenge akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani 2020-2025 , alieleza mkoa unatarajia kupata bilioni 314 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji .
“Upatikanaji wa maji safi na salama umetokana na kukamilika kwa miradi 26 iliyotekelezwa 2019-Juni 2021″Miradi mitano ya bilioni 3.930.685 ni mipya na miradi 21 inafanyiwa ukarabati kwa gharama milioni 651.502.112 kwa jumla miradi hii itanufaisha wakazi 28,889”
Kunenge alieleza,bajeti 2021-2022 jumla ya bilioni 17.916.266.5 kupitia mfuko wa maji program ya lipa kwa matokeo na serikali kuu zimetengwa kwa ajili ya miradi 94.
Sekta ya maji imekuwa na mafanikio mkoani Pwani kutokana na kufikia wananchi kwa asilimia 72 vijijini na asilimia 84 mijini .