********************
Na WAMJW
Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imemtambua Mwanariadha Michael Filberth Nondo, mkazi wa Kigoma aliyejitolea kutembea kutoka mkoani Kigoma mpaka mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu ugonjwa wa UVIKO-19 na kuchanja Chanjo dhidi ya Uviko -19.
Katibu Mkuu Wizara ya ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi, ameueleza Umma kupitia Vyombo vya Habari akimwakilisha Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima jijini Dodoma.
“Kama Serikali tunatambua juhudi zinazofanywa na wadau mbali mbali katika Mapambano haya ya Corona, lakini kwa leo kama Wizara niseme, tumetambua ndugu Michael Nondo, aliye onesha Ujasiri na Uzalendo wakutembea kutoka mkoani Kigoma mpaka mkoani Kilimanjaro ikiwa ni sehemu yakuunga Mkono juhudi zinazo endelea nchini kote.” Amesema Prof. Makubi.
Kwa kutambua Mchango wake, Prof. Makubi amemkabidhi Cheti na kumpa hadhi ya ukamanda wa Kuhamasisha Wananchi kupata Chanjo kwa kuthamini mchango na uzalendo wake katika kampeni hiyo ya uchanjaji.
Kwa upande wake, mwanariadha huyo amesema, sababu kubwa iliyo msukuma kufanya zoezi hilo ni imani aliyonayo juu ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na sekta zote ikiwemo sekta ya Afya katika Mapambano dhidi ya Uviko- 19.
Hii ni mara ya pili kwa Nondo, kufanya safari hiyo baada ya kufanya zoezi kama hilo mwezi wa sita Mwaka huu kwa mara ya kwanza, kisha kujipumzisha kwa miezi miwili kabla ya kurudia tena awamu hii,
“Mara ya kwanza kufanya safari hii nilikuwa nikifanya usiku lakini hivi sasa nimeamua kufanya mchana ili kila mmoja anione, ninawashukuru sana Serikali hususan ngazi za Serikali za mitaa nilipoweza kupita ambapo walinipa sehemu za kulala na kunikutanisha na wananchi, kunitambulisha na kuongea nao kwa lengo la kutoa Elimu juu ya ugonjwa huu” amesema Nondo
Ametoa wito kwa vijana, watu wa makamo na wazee kwenda kupata chanjo kwa hiari kwa sababu chanjo hiyo haina madhara na kushauri kuacha kusikiliza tetesi zisizokuwa za kweli na zenye lengo la kupotosha.
Amewataka watanzania wajue kuwa Taifa linawahitaji kwaajili ya kujenga Taifa hivyo kujitokeza kupata Chanjo pamoja na kuchukua tahadhari za Maradhi ikiwepo UVIKO-19 ni muhimu sana kwao.