……………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani , Aboubakari Kunenge ,ametoa onyo kwa baadhi ya mabaraza ya ardhi mizigo ,ambapo amedai mabaraza hayo yatapimwa kwa kazi zao na hatosita kuyavunja yale mabaraza yasiyowajibika.
Kunenge amesema amejipanga kuyasafisha mabaraza yasiyofanya kazi zake ipasavyo na yanayopindisha sheria na kutotenda haki.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ( 2020-2025), katika mkutano wa halmashauri Kuu ya CCM mkoa ,Kunenge alisema , wajumbe wasiotimiza wajibu wao bila kutenda haki wanaondoa imani kwa wananchi.
Hata hivyo alisema ,wajumbe wa mabaraza hayo wapo kwa ajili ya kutatua migogoro haiwezekani, walengwa kwenda mkoa wakati mabaraza hayo yapo ,na Kama wapo mizigo waondolewe.
Pia Kunenge alifafanua ,wapo watu wanaokwamisha maendeleo kwa kupitia mwamvuli wa chama ,na ameomba wasaidiane na chama kuchukua hatua kwa watu hao.
“Migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya ardhi inakuwa mingi kutokana na kutofuata sheria”alisisitiza.
Katika hatua nyingine,mkuu wa mkoa huyo alisema migogoro ya ardhi ni muiba katika mkoa huo ,Ni changamoto inayomnyima usingizi .
Kunenge alieleza utekelezaji upo vizuri kwa sekta zote na changamoto zilizopo serikali inaendelea kuchukua hatua kuboresha na kutatua.
Nae Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani,Ramadhani Maneno alieleza wapo kwenye mahusiano mazuri na serikali Mkoa .
Maneno pia aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu,kwa maendeleo ya mkoa huo na kusema wataendelea kumuunga mkono.
Akizungumzia masuala ya chanjo ya Uviko 19 ,mganga mkuu wa mkoa wa Pwani,Dokta Gunini Kamba alisema zaidi ya watu 15,000 wameshachanja mkoani Pwani.
Gunini alieleza , hali ni ya kuridhisha licha ya kuomba wananchi wakachanje kwa hiari yao kwani chanjo hiyo inasaidia na haina madhara yoyote.
“Tumekuja kuongea na halmashauri Kuu , tushirikiane kuhamasisha zoezi hili ili kupambana na ugonjwa huu ,ugonjwa upo ,tujihadhari “alisisitiza Gunini.